KAMATI ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imelishauri Bunge wakati wa utungaji Sheria ya Fedha ya Mwaka 2017 kuongeza tozo kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli.
Nia ni kupatikana fedha kwa ajili ya Mfuko wa Taifa wa Maji, ili kugharimia miradi ya maji nchini.
Ilisema tozo hiyo iwe Sh 100 badala ya Sh 50 kwa sababu Mfuko huo umeonesha mafanikio makubwa katika kuwezesha upatikanaji fedha licha ya kiasi kinachopatikana kutokidhi mahitaji ya maji yaliyopo.
Akiwasilisha taarifa ya shughuli zilizotekelezwa na Kamati hiyo mwaka 2016 hadi 2017, Mwenyekiti wake Dk Christine Ishengoma alisema: “Kamati inashauri kuongeza tozo kutoka Sh 50 hadi Sh 100 kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli.”
Alibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kupatikana fedha za kutosha kugharimia miradi ya maji.
Alibainisha kuwa Kamati hiyo ilibaini kuwa katika Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2016/17, katika fungu la fedha za maendeleo, Serikali ilitenga kiasi kikubwa cha fedha za ndani ikilinganishwa na fedha za nje, ambazo hazikutolewa.
“Hazitolewi kama zilivyoidhinishwa na Bunge, hivyo kuchangia kutofikiwa kwa malengo yaliyopangwa,” alisema Dk Ishengoma.
“Hili si jambo dogo katika utekelezaji wa mipango ya Serikali, linahitaji ufumbuzi, la sivyo bajeti ya Serikali katika miradi ya maendeleo itaendelea kuwa kiini macho,” alisema.
Alibainisha kuwa upatikanaji wa fedha za ndani za miradi ya maendeleo kwa kipindi cha nusu mwaka zilizokuwa zimetolewa; kilimo kilipangiwa Sh bilioni 22 lakini mpaka wakati huo kilikuwa hakijatolewa kiasi chochote.
Kwenye Mifugo na Uvuvi, ilipangwa Sh. bilioni 8, lakini zilitolewa Sh milioni 280 huku Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ikipewa Sh milioni 767 kati ya Sh bilioni 6.
Wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wake, Atashasta Nditiye alisema Kamati hiyo ilibaini changamoto ndani ya Mamlaka ya Wanyamapori nchini, ikiwa ni pamoja na mbinu mpya ya ujangili.
“Kuna mbinu mpya ya ujangili ambapo majangili wanatumia sumu kuua wanyamapori. Mbinu hii ni hatari, kwani wanaua wanyamapori wa aina mbalimbali, hata wasiokusudiwa,” alisema Nditiye.
Kamati hiyo ilishauri Serikali kuajiri watumishi wa kutosha wenye ujuzi na utaalamu wa kisasa hasa askari wa wanyamapori.
“Pia kutatua migogoro ya mipaka ya hifadhi na vijiji vinavyopakana na hifadhi kwa kushirikiana na wananchi. Serikali iondoe wafugaji kwenye hifadhi zetu ili kunusuru hifadhi na mazingira,” alisema.