“Usione vyaelea vimeundwa.” Huo ni msemo wa wahenga unaomaanisha kila mafanikio yana maandalizi yasiyo ya kubahatisha.
Msemo huo unaendana na kilichotokea katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa wiki hii, ambayo katika shule 10 zilizofanya vizuri hakuna hata moja yenye maandalizi ya lele mama. Shule nyingi kati ya hizo ada zake ni kuanzia Sh8 milioni hadi 10 kwa mwaka.
Uchunguzi umebaini kuwa shule hizo zote ni zenye majengo mazuri, walimu wazuri na wenye motisha, maabara zilizokamilika, sehemu nzuri za kulala na zinazotoza ada zaidi ya Sh2.5 milioni, mbali ya gharama nyingine za chakula, malazi na vitabu.
Shule 10 zenye watahiniwa zaidi ya 40 zilizoshika nafasi za kwanza ni Feza Boys (Dar es Salaam), St. Francis Girls (Mbeya), Kaizirege (Kagera), Marian Girls (Pwani), Marian Boys (Pwani), St Aloysius Girls (Pwani), Shamsiye Boys (Dar es Salaam), Anwarite Girls (Moshi), Kifungilo Girls (Lushoto) na Thomas More Mashrina (Dar es Salaam).
Wanafunzi wa Sekondari Kaizirege Junior iliyoshika nafasi ya tatu, kila mmoja analipa Sh2.5 milioni za ada. Malipo hayo kwa baadhi ya shule hayahusishi gharama za malazi, chakula na vitabu.
Shule ya Wasichana ya St. Francis ili mwanafunzi ajiunge nayo, anatakiwa kulipa Sh2.2 milioni za ada kwa mwaka, huku akitakiwa kulipa katika mikupuo minne mbali na mahitaji mengine.
Mwanafunzi wa Feza Boys ada ni Sh2.9 milioni, lakini ikijumlishwa na gharama za chakula, malazi na vifaa vya masomo, inafika zaidi ya Sh8 milioni.
Kuhusu Thomas More Machrine ada ni Sh3.6 milioni kwa kidato cha nne na cha sita. Hivyo, mwanafunzi akisoma kwa miaka minne anatakiwa kulipa Sh14.4 milioni.
Uchunguzi huo ulibaini mwanafunzi anayesoma shule za Marian Boys na Girls kidato cha kwanza hadi cha nne, anatakiwa kulipa Sh2.8 milioni.
Kwa wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo kwa ajili ya kidato cha tano na sita, watalipa Sh2.7 milioni hiyo ina maana watatakiwa kulipa Sh5.4 milioni kwa miaka miwili.
Shule ya Anwarite ya Kilimanjaro ada yake ni Sh1.9 milioni, hivyo kwa miaka minne mwanafunzi analazimika kulipa Sh7.6 milioni.
Mmoja na viongozi wa shule hizo ambaye hakuwa tayari kutajwa, alisema shule hizo zinatoa elimu bora na mazingira mazuri ya kuishi kwa mwanafunzi, hivyo badala ya kuonekana kero zingepewa ruzuku.