RAIS John Magufuli amesema serikali haitajishughulisha na Watanzania waliokamatwa ughaibuni na kuhukumiwa kunyongwa kutokana na kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
Huku akianika orodha mpya yenye maelfu ya Watanzania walio kwenye magereza ya ughaibuni tofauti na iliyotajwa Ijumaa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Magufuli alisema hukumu dhidi yao zinapaswa kutekelezwa na Tanzania haitahusika kuwatetea.
Rais Magufuli alituma 'salamu' hizo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuwaapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Dk. Anna Peter na mabalozi watatu.
Rais aliwataka mabalozi wa Tanzania walioko katika nchi mbalimbali kutojihusisha kwa vyovyote na wafungwa wa makosa ya madawa ya kulevya.
"Watanzania waliohukumiwa nje ya nchi kwa kujihusisha na dawa za kulevya, mabalozi msijihusishe nao... waacheni," Rais Magufuli alisema.
"Kama wamefungwa kifungo cha maisha, waacheni wafungwe, kama wamehukumiwa kunyongwa, wanyongwe tu.
Tukichekacheka, taifa litaathirika na dawa za kulevya." Alisema idadi ya Watanzania waliokamatwa na dawa za kulevya nje ya nchi inatisha kutokana na idadi aliyopatiwa.
Alisema orodha yake inahusisha nchi 17 zenye jumla ya Watanzania 663 huku China ikiongoza kwa kuwa na wafungwa 268 wa dawa za kulevya kutoka nchini.
Rais Magufuli alisema Msumbiji kuna Watanzania 20 waliofungwa baada ya kukamatwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya, Nepal (wanne), India (26) na 268 walioko kwenye magereza ya China.
Nchi nyingine, alitaja Rais Magufuli ni Uturuki (38), Ugiriki (25), Malaysia (16), Indonesia (mmoja) Comoro(watatu), Pakistan (watatu), Japan (60), Nigeria (91), Ghana (mmoja), Uingereza (24), Kenya (66), Misri (wawili) na Uganda (15).
Rais Magufuli alisema vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake.
Alisema serikali imepewa jukumu la kupambana na kutokomeza biashara ya dawa za kulevya kwa mujibu wa sheria namba tano ya mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge la 10 na kusainiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete Mei 11, 2015.
"Ninamshukuru sana Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kuisaini sheria hiyo pamoja na wabunge," alisema Rais Magufuli na kubainisha: "Kifungu namba 10 katika sheria hiyo kinaeleza mwenye jukumu la kupambana na dawa za kulevya ni serikali."
Alisema alishangazwa kuona hadi Ijumaa alikuwa hajaletewa jina la Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya uteuzi, na kulazimika kumteua kamishna anayemfahamu mwenyewe.
"Unaweza kuona vita hii ilivyokuwa ngumu, hata jina la kamishna mpya ambaye nilipaswa kuletewa ili nimteue lilifichwa," alisema Rais Magufuli.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema pia yeye hakuwa ametaarifiwa kuwa anatakiwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya na kwamba ili kufanikisha vita dhidi ya dawa za kulevya, Kamishna Mkuu aliyeapishwa anapaswa kushirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama na wajumbe wa baraza la kudhibiti dawa za kulevya.
Alisema wajumbe wa baraza hilo, ambao pia hakuwa na taarifa, ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.
Wengine ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
WATU 65 Majaliwa alisema serikali haitamwachia mtu yeyote atakayekamatwa na dawa za kulevya hata kama ni 'kigogo'. Alisema kwa mwaka 2016, serikali ilikamata bangi tani 3.4 na kuwapo kwa kesi 934 mahakamani, mirungi tani 1.8 na kesi 135, heroine kilo 50.5 kesi 292, na cocaine kilo 5.4 zenye kesi nne mahakamani.
Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini imepata msukumo mpya tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ataje orodha ya watu 65 ambao alitaka waisaidie polisi kuhusu biashara ya madawa ya kulevya Jumatano.
Kabla ya kutaja orodha hiyo iliyokuwa na viongozi wa dini, wafanyabiashara na wanasiasa, Makonda alikuwa ametoa orodha ya Polisi 12 na wasanii kadhaa ambao walitakiwa pia kufika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano.
Lakini harakati za kuwakamata watumiaji, wauzaji na watu wenye taarifa kuhusu biashara ya dawa za kulevya katika jiji la Dar es Salaam ilipata msukumo mkubwa mwanzoni mwa wiki iliyopita baada ya Rais Magufuli kutaka zisiache mtu yeyote.
“Hakuna mtu maarufu, mwanasiasa, waziri au kiongozi yoyote au mtoto wa fulani, askari ambaye anajihusisha na dawa za kulenya aachwe, hata awe mke wangu Janeth... kamata wote weka ndani,” alisema Rais Magufuli.
Alisema biashara ya dawa za kulevya kwa sasa nchini imefikia katika hali mbaya na kwamba zinauzwa kama njugu nchini. Alitaka vyombo vyote vya ulinzi vinavyoendelea kupambana na dawa za kulevya viendelee na mapambano.
Alisema biashara ya dawa za kulenya kwa sasa nchini inapoteza nguvu kazi za Watanzania wengi haswa vijana, na kwamba vyombo vyote vya ulinzi vinapaswa kushirikiana ili kuwakamata hao.
Rais Magufuli aliwataka wahusika kuuwinda mtandao wote unaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya. “Haiwezekani wauzaji wapo mtaani wanatanua tu, hawakamatwi," alisema Rais Magufuli.
"Kwa mfano kuna muuzaji mkubwa yupo mkoani Lindi, alishikwa na dawa za kulevya, lakini sijasikia hata siku moja akitangulizwa Mahakamani.
"Ninajua kuna viongozi wanamtetea.” Rais Magufuli alikuwa akimzungumzia mtu anayeaminika kuwa 'mzungu wa unga' aliyekuwa akitafutwa zaidi nchini.
Ali Khatibu Haji (47), maarufu kwa jina la Shikuba, alikamtwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Machi, 2014 baada ya kuwindwa kwa miaka miwili kabla ya kuhamishiwa mkoani Lindi.
Anatuhumiwa kuwa kiongozi wa genge lenye makao yake Afrika Mashariki, lakini likiwa na uhusiano wa kibiashara mpaka China, Brazil, Canada, Japan, Marekani na Uingereza.
Rais Magufuli alimwagiza Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuhakikisha kesi zote zinazohusu dawa za kulevya zinasikilizwa haraka.