BARAZA la Wawakilishi Zanzibar (BLW) limepitisha sheria mpya ya Bendera ya Zanzibar, Nembo ya Serikali na Wimbo wa Taifa ambapo wasanii na wafanyabiashara wamepigwa marufuku kuvitumia kwa matangazo ya biashara.
Muswada wa sheria hiyo uliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed.
Akifunga mjadala wa muswada huo, Waziri Aboud alisema serikali imeamua kuweka utaratibu mzuri wa kisheria wa kutumia Bendera ya Zanzibar, Nembo ya Serikali na Wimbo wa Taifa wa Zanzibar.
Alisema wanamichezo na wasanii wataruhusiwa kutumia Bendera ya Zanzibar wanapokua katika mashindano, yakiwemo ya kimataifa katika kuendeleza na kuimarisha utaifa.
“Nembo ya Serikali ni alama nyeti (hivyo ni) marufuku kutumika kwa matangazo," alisema Waziri Aboud. Marufuku hiyo inahusu pia Bendera ya Zanzibar.
Alisema baada ya sheria hiyo kupitishwa, kutatungwa kanuni ambazo zitaweka utaratibu mzuri wa matumizi yake, ambapo pamoja na mengine shule za umma na binafsi zitatakiwa wanafunzi wake kuimba wimbo wa taifa kila siku.
Waziri Aboud alisema Bendera ya Zanzibar itakuwa ikipandishwa saa 12 asubuhi na kuteremshwa saa 12 jioni na wakati ikiteremshwa wananchi katika maeneo husika watatakiwa kuheshimu, ikiwemo kusimama kwa muda.
Alisema sheria hiyo itasadia kujenga uzalendo na umoja wa kitaifa na viwango vya ubora vya kitambaa cha Bendera ya Zanzibar kitazingatiwa kama walivyopendekeza wajumbe wa Baraza hilo.
Hata hivyo, wakichangia mswaada huo baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipinga marufuku ya kutumia bendera na wimbo kwa matangazo ya biashara.
Wajumbe waliopinga ni Hassan Hafidh Khamis (Welezo), Simai Mohamed Said (Tunguu), Suleiman Sarahan (Chakechake), na Ali Suleiman Ali (Kijitoupele).
Walisema bendera kutumika katika matangazo ya biashara na kazi za sanaa kunasadia kuitangaza nchi pamoja na kuongeza uzalendo na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake.
Simai alisema zipo nchi nyingi duniani zinatumia bendera za nchi zao katika kuitangaza nchi kupitia bidhaa wanazozalisha, kazi za sanaa na michezo.
“Mheshimiwa Spika, kama wamasai wanatengeneza vitu vya mapambo na kutumia rangi za Bendera ya Taifa, wanatangaza nchi na kuonyesha uzalendo wao; kwanini Zanzibar wafanyabiashara na wasanii wazuiwe?” Alihoji Sarahan.
Sarahan alisema wananchi wanapoipenda nchi yao hufikia hata kujifunga bendera kiunoni, kichwani na kucheza ngoma, na wengine hata kufikia kutandika na kulala juu ya bendera.
Mwakilishi Jaku Hashimu Ayoub alitaka kufahamu kama kuwapo kwa nyimbo mbili za taifa si kuleta mkanganyiko nchini.
“Mheshimiwa Spika mie elimu yangu ndogo ndiyo maana sijateuliwa kuwa waziri wala Naibu Waziri, naomba kuelimishwa inakuwaje kuwapo wimbo wa Taifa na wa Zanzibar?” Alihoji Jaku.