A - Z ya Kisa cha Kutumbuliwa Katibu wa Wizara ya Nihati na Madini,Kumbe Alibishana Kuhusu Agizo Hili la Rais Magufuli,Yasemekana Kigogo wa Bandari Alimchongea kwa Magufuli..!!!


KATIBU Mkuu wa Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa jana alibishana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko wakati Spika wa Bunge akiwa kwenye ziara kwenye Bandari ya Dar es Salaam kukagua makontena yanayodaiwa kuwa na madini.

Muda mfupi baadaye, taarifa ya 'kutumbuliwa' kwa Prof. Ntalikwa aliyeteuliwa Desemba mwaka 2015, ilitolewa kupitia taarifa ya Ikulu.

Taarifa hiyo ilisema nafasi hiyo itajazwa baadaye.

Wawili hao walitofautiana kuhusu mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kujua kilichomo ndani ya makontena 256 ya 'mchanga' wa dhahabu (concetrates) yanayoshikiliwa na TPA kufuatia marufuku ya Rais Magufuli ya kuyasafirisha nje.

Hadi sasa kampuni za madini zinadai ndani ya makontena hayo na mengine 20 ambayo Rais Magufuli alionyeshwa katikati ya wiki iliyopita yote yakiwa kwenye hatua za mwisho za kusafirishwa kuna mchanga, lakini TPA inasema kuna madini.

Baada ya Spika na Kamati yake kuelezwa jinsi kontena hizo zilivyokamatwa, ndipo kila upande ulipotoa ushauri wa namna ya kulikabili suala hilo.

Aliyekuwa Katibu Mkuu huyo alitoa ushauri ambao ulionekana kupingana na maelezo ya Mhandisi Kakoko ambaye alidai ana uhakika wa asilimia 90 kuwa kilichomo kwenye kontena hizo ni madini na siyo mchanga.

Prof. Ntalikwa, kwa upande wake, alishauri kuunda timu ya wataalamu kutoka sekta mbalimbali kuchunguza suala hilo.

Alishauri kuchukuliwa kwa sampuli na kuzipeleka maabara na kujua ukweli.

“Mheshimiwa Spika, napendekeza tutengeneze timu ya wataalamu kuchukua sampuli na kuzipeleka maabara kupima," alisema Prof. Ntalikwa. "Timu hiyo inaweza kujumuisha taasisi nyingine, alafu taarifa iwekwe wazi kwa umma.”

Ushauri huo haukumfurahisha Kakoko ambaye moja kwa moja alisema anaandaa barua kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) na Wizara waeleze kwa kina juu ya suala hilo na kwamba linahitaji kujipanga sana ili kuliendea.

“Katibu Mkuu wewe labda ni mgeni, haya masuala huyajui vizuri," alisema Kakoko.

"Vipimo vinafanyika lakini humu kuna jambo la ziada, hatuwezi kuliendea hili jambo kwa ‘theory’ (nadharia) bali ‘practical’ (vitendo) zaidi.

"Twende hadi kwenye migodi tuone wanavyochukua sampuli, zinavyopimwa na kule unapopelekwa China, Ujerumani na kwingine tujue matokeo ya vipimo vyao, vinginevyo hatutafanikiwa.”

Alisema kwa sasa kila kontena linaloingia bandarini humo lazima lipite kwenye mashine maalum kujua kilichomo, na kwamba wameongeza mashine sita za 'scan' ili kuongeza ufanisi zaidi.

Baada ya ziara hiyo, Ndugai na wabunge hao walitoa majumuisho na kueleza kuwa Bunge litaunda kamati ya kuchunguza mikataba, sheria na mchakato zima wa sekta ya madini, ikiwamo kujua kilichomo kwenye makontena 256.

Ripoti ya kamati hiyo, alisema Ndugai, itaishauri serikali kama iendelee na biashara ya kusafirisha 'mchanga' huo au la.

Alipoulizwa  mbele ya Spika, wakati wa chakula cha mchana ana uthibitisho gani kuwa ndani ya makontena kuna madini na si 'mchanga', Mhandisi Kakoko alisema “Sisi ni watendaji wa serikali.

"Tumeshafanya uchunguzi wetu na kubaini kuwa ndani ya makontena yale kuna madini ya dhahabu kwa asilimia 90.”

Ziara ya Spika na wabunge imetokana na matokeo ya ziara ya kushtukiza bandarini hapo ya Rais Magufuli ambapo alionyeshwa makontena 20 ya kampuni ya Acacia ya 'mchanga' wa dhahabu, yakisubiri kusafirishwa nje ya nchi kinyume na maelekezo ya yake Machi 2.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMA), Gilay Shaonika, alieleza wabunge hao kuwa uchukuaji wa vipima ufanyika mgodini na ripoti kutumwa bandarini na baadaye hulinganishwa na itakayotoka nje ambako 'mchanga' huo umepelekwa.

Alisema kila kontena la mchanga huo huwa na asilimia 0.02 ya madini yoyote, jambo ambalo lilipingwa na Spika na kueleza hakuna mwekezaji atakayefanya biashara ya faida hiyo ikiwamo gharama kubwa za kusafirisha mchanga huo.

“Hakuna mwekezaji anaweza kufanya bishara kama hii kwa faida ya 0.02," alisema Spika Ndugai.

"Lipo tatizo; ndiyo maana tunataka tufanye uchunguzi nasi tuweze kuishauri serikali iendelee na biashara hii au la.

"Nani analinda maslahi yetu mchanga unapofika Ulaya na kupimwa, au tunasubiri ripoti zao?”

Kauli ya TMA ilipingwa na Mhandisi Kakoko pia, ambaye alisisitiza kuwa na uhakika asilimia 90 ya kilichomo kwenye kontena hizo ni madini na siyo asilimia 0.02 ya madini kama inavyoelezwa.

Baada ya kauli hiyo, Spika alimhoji mwakilishi wa TMAA “kwa kufikiri kwako unadhani kuna mwekezaji anaweza kufanya biashara kwa faida ya 0.02? Atoe gharama za meli, usafiri na bandari.”
Alijibu haiwezekani.

“Ni lazima tufanye uchunguzi kujua hii biashara inaendeshwaje na ni nani ananufaika nayo," alisema zaidi Ndugai.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad