Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametekeleza mambo manane mapya ambayo hayakuwamo kwenye orodha ya ahadi zake za mwaka jana wakati alipoingia madarakani.
Siku chache baada ya kuapishwa, Makonda alikutana na wenyeviti wa Serikali za mtaa na kuwaeleza mikakati tisa aliyopania kuifanya katika kulibadilisha Jiji la Dar es Salaam.
Jumatano iliyopita, Makonda aliadhimisha mwaka wake mmoja tangu ateuliwe kushika wadhifa huo akielezea mambo 10 aliyoyafanya katika kipindi hicho na mengine 10 atakayoyafanya katika mwaka wake wa pili.
Wachambuzi wa masuala ya sayansi ya siasa wamempongeza kiongozi huyo na kusema hata kama hajatimiza baadhi ya ahadi, lakini amekuwa mbunifu kwa kujifanyia tathmini ukilinganisha na viongozi wengine.
Mipango aliyotekeleza
Mambo aliyotekeleza ambayo hayakuwamo kwenye orodha ya mikakati yake ni kampeni ya mti wangu, ujenzi wa wodi ya wagonjwa, vita ya dawa za kulevya, ujenzi wa ofisi ya Bakwata, kampeni ya uchangiaji wa damu, marufuku ya shisha na migogoro ya ardhi.
Ahadi tisa za 2016
Wakati alipoingia madarakani na kuzungumza na wenyeviti wa Serikali za mtaa, Makonda aliahidi usafi wa jiji, ofisi za Serikali kutokuwa za chama, kutenga maeneo ya biashara, sensa ya nyumba kwa nyumba, usalama wa raia na mali zao, watumishi hewa, kurudisha hadhi ya watendaji wa Serikali za mitaa, elimu na barabara.
Kwenye suala la usafi, Makonda aliahidi zawadi ya gari la Sh20 milioni au fedha taslimu kwa mwenyekiti ambaye mtaa wake utaongoza kwa usafi na Sh5 milioni kwa kila mjumbe wa mtaa husika. Pia, alisema zawadi hiyo itakayokuwa ikitolewa kila baada ya miezi mitatu na kwamba ingeanza Aprili Mosi, 2016.
Licha ya kusema kuwa amefanikiwa kufanya mambo kumi, Makonda ameshindwa kutekeleza ahadi tisa za mwaka jana alizoahidi mwaka jana.
Kuhusu usalama
Mwaka jana, Makonda aliahidi kutoa pikipiki 30 kwa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam ili kuwawezesha askari kuwafuatilia watu watakaotupa taka ovyo barabarani.
Kwenye suala la usalama wa raia na mali zao, kiongozi huyo alisema kila mwenyekiti wa mtaa anapaswa kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama na hilo litafanikiwa endapo atakuwa na utaratibu wa kujua nani anafanya nini.
Ofisi za Serikali
Suala la ofisi za Serikali kuwa za chama, mkuu huyo wa mkoa alisema ofisi za Serikali ni kwa ajili ya kazi na siyo sehemu ya kufanyia siasa akisema katika uongozi wake haangalii chama, bali kusikiliza matatizo ya kila mtu.
Kutenga maeneo ya biashara
Katika kutenga maeneo ya biashara, Makonda alisema matamanio yake ni kuiona Dar es Salaam ya kisasa ambayo itakuwa na maeneo maalumu kwa ajili ya biashara ya vileo, magari, gereji na vifaa vya ujenzi.
Aliwaagiza wakurugenzi wa manispaa ifikapo Mei Mosi wawe wameainisha maeneo maalumu kwa ajili ya biashara hizo.
Barabara za biashara
Makonda aliahidi kuzungumza na wakurugenzi wa manispaa ili kuangalia namna ya kuandaa utaratibu wa kutenga barabara moja kwa kila kata kwa siku moja ili watu wafanye biashara.
Sensa ya wakazi wa Dar
Katika suala la sensa nyumba kwa nyumba aliwataka wenyeviti wa mitaa kupita kila nyumba katika mitaa yao kuorodhesha idadi ya watu wanaoishi na shughuli zao.
Alisema hiyo itasaidia pia kujua watu wasiokuwa na ajira hivyo kujipanga namna ya kuwasaidia.
Ahadi kwa polisi
Aliahidi kutoa Sh1 milioni kwa polisi atakayepambana na majambazi, huku milioni moja nyingine ikienda kwa mtu atakayesalimisha bunduki au bastola kituo cha polisi.
Watumishi hewa
Akizungumzia watumishi hewa, alitoa agizo: “Nitakapoagiza orodha ya watumishi hewa ije kamili, kinyume na hapo ofisa utumishi atalazimika kulipa hata madeni yaliyopita maana anaonekana ana nia ya dhati ya kufuga uozo huo.”
Ofisi za watendaji wa mitaa
Makonda pia aliwaahidi kuwajengea ofisi wenyeviti wote wa Serikali za mitaa na kuachana na habari za kupanga na kwamba, ifikapo Aprili Mosi atawakopesha pikipiki 1,000 ili ziwasaidie katika utendaji wao wa kazi na kuwasaidia kujikimu kimaisha.
Barabara
Kuhusu kero ya barabara, aliahidi kuzishughulikia, huku akiwashangaa wahandisi kwa kukaa ofisini.
Mafanikio 10 aliyotaja
Baada ya mwaka mmoja, mkuu huyo wa mkoa alibainisha mambo aliyoyafanya ndani ya mwaka huo mmoja.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuendesha kampeni ya mti wangu inayohamasisha upandaji miti, ujenzi wa wodi za wagonjwa, vita dhidi ya dawa za kulevya na kutatua migogoro ya ardhi kwa wananchi.
Mambo mengine aliyoyafanya ni ujenzi wa Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), kampeni ya kuchangia damu, utengenezaji wa madawati kwa ajili ya shule za umma, uhakiki wa silaha, usafi wa jiji na kupiga marufuku matumizi ya shisha.
Ahadi mpya 10 alizotoa
Makonda alibainisha pia mambo mengine 10 atakayoyafanya katika mwaka wake wa pili wa uongozi akianza na kusimamia watumishi wa umma kutekeleza wajibu wao katika ngazi ya Serikali za mitaa mpaka ya mkoa.
“Nitapita kuanzia ngazi ya Serikali za mtaa na kila mtendaji atanieleza namna anavyowahudumia wananchi. Wananchi wanakuja mpaka ofisi ya mkuu wa mkoa kuleta kero zao wakati zinaweza kutatuliwa kwenye mitaa yao, hatuwezi kwenda namna hiyo,” alisema.
Makonda ambaye amejipatia umaarufu zaidi kutokana na vita dhidi ya dawa za kulevya, alisema atahakikisha kwamba anawahudumia waathirika wa dawa hizo kwa kuwapatia tiba ya uraibu wao.
Kuhusu wakazi wa mabondeni, alisema atahakikisha wote wanaoishi katika maeneo hayo wanahama na tayari ameagiza nyumba zao kubomolewa kwa ajili ya kulinda usalama wao.
Alisema wakazi waliopewa viwanja katika maeneo hayo ambao wana hati za viwanja hivyo, atawapatia ardhi sehemu nyingine kwa sababu ni uzembe wa watendaji wa Serikali na kusisitiza kwamba watakaobainika kuhusika na uzembe huo watawajibishwa.
Asifiwa wa wasomi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema hadi hapo Makonda ameonyesha ushujaa kwa kuwa mkuu wa mkoa wa kwanza kuelezea utekelezaji wa ahadi zake. “Ingekuwa ni kugawa medali kijana huyu angepata licha ya makandokando yanayomzunguka, amefanya kazi nzuri, amethubutu na ni mbunifu,” alisema.
Alisema kwenye utendaji wa kazi jijini Dar es Salaam, kiongozi huyo wa mkoa anasikika zaidi katika uchapaji wa kazi kuliko viongozi wa kuchaguliwa wakiwamo wabunge na mameya.
Hata hivyo alisema ni wakati wa viongozi wengine kujitathmini na kuelezea yale waliyoyafanya.
Kuhusu ahadi ambazo hajazitekeleza, Dk Bana alisema muda bado na kwamba, ikiwa atadumu kwenye nafasi hiyo huenda utekelezaji wa ahadi zake ungekuwa juu zaidi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema mara nyingi viongozi huwa wanatekeleza mipango ambayo haikuwepo kwenye ratiba zao kutokana na kuibuka ghafla au umuhimu wake.
Alisema ni afadhali Makonda kwa kuwa ameonyesha kwa vitendo hata kama hakutimiza ahadi zake za awamu iliyopita kuliko, kukaa kimya bila kujifanyia tathmini ulikofanikiwa na kushindwa.
“Hatua ya kujifanyia tathmini naweza kusema ni ya kishujaa, wakuu wa mikoa wengine wanaweza kuiga hii itawafanya watimize yale wanayoyapanga na hivyo kuwaletea wananchi maendeleo,”alisema.
Mchambuzi wa uchumi mkoani Arusha, Dk Godwin Maimu alisema hatua ya kiongozi huyo kujitathmini ni nzuri japo anapaswa, kutekeleza ahadi zake kwa wananchi licha ya kuwa si kiongozi wa kuchaguliwa.
“Bado jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na tatizo la wamachinga kutengewa maeneo kwa ajili ya biashara, amejitahidi lakini lazima awe na vipaumbele kwa masuala ya msingi anayodhani atayatekeleza,” alisema.