Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Venance Mabeyo amesema Jeshi lake lipo tayari kupunguza deni linalodaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Bilioni 3, huku akiahidi kesho Jumatatu kuanza kwa kupunguza deni hilo.
Akizungumza na waandishi wa Habari Makao Makuu ya Jeshi (Ngome) Jijini Dar es Salaam amesema deni hilo limetokana na matumizi makubwa ya umeme, ukubwa wa jeshi lenyewe na mgawanyiko wake nchi nzima, zana wanazotumia huku nyingine zikilazimika kuwashwa muda wote kwa saa 24 kwa lengo la kulinda na kuimarisha ulinzi wa Taifa.
"Baada ya kupokea maelezo ya Tanesco na kufuatia tamko la Rais, Jeshi la Wananchi limetafakari na limefanya jitihada kupata fedha za kupunguza deni hili, tunadaiwa fedha kiasi kinachozidi kidogo Sh3 bilioni na Tanesco peke yake, tayari nimeagiza watendaji wetu watafute kiasi cha Sh 1 bilioni na wahakikishe kesho Marchi 27, cheki inawafikia Tanesco haraka ili huduma hiyo iendelee kutumiwa." Alisema Mabeyo
Pamoja na hayo Mkuu huyo amesema ufinyu wa bajeti umekuwa changamoto kubwa kwao katika kukabiri mahitaji makubwa katika jeshi hilo.
Kwa upande mwingine Mabeyo ameshauri na kusisitizia kwa Taasisi nyingine za Serikali kulipa deni ili kuongezea Tanesco uwezo wa kutoa huduma bora zaidi sekata za utumishi pamoja na kwa wananchi kwa ujumla ambao mpaka sasa wanashida ya umeme.