BAADA ya kimya kirefu cha tangu mwishoni mwa mwaka 2015, waziri mstaafu wa serikali ya awamu ya nne, Prof. Mark Mwandosya, amezungumza kutoka kijijini kwake Lufilyo, katika Halmashauri ya Busokelo, mkoani Mbeya.
Katika salamu zake alizozitoa jana, Prof Mwandosya alitaka vyuo vikuu na taasisi za sayansi na teknolojia kurekebisha uwiano ulio hasi katika usaili wa wanafunzi wa kike, katika fani na masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.
Katika salamu hizo, Prof. Mwandosya ambaye alikuwa mmoja wa watia nia 40 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 pia alipendekeza juhudi za kuhamasisha wanawake kupenda masomo ya sayansi zihusishe wahadhiri.
Alisema wahadhiri hao wanapaswa kutembelea shule za sekondari na kufanya mazungumzo na walimu na wanafunzi wa kike.
Prof. Mwandosya alisema mazungumzo hayo yalenge katika kufafanua misingi na nguzo za sayansi na hisabati na kuwashawishi wanafunzi, hasa wa kike, kutoogopa kuchukua michepuo yenye masomo ya sayansi na hisabati.
“Maendeleo ya taifa lolote line yanatokana na matumizi bora ya sayansi na teknolojia. Hivyo basi ajira nyingi pia zinatokana na matumizi ya sayansi na teknolojia katika maendeleo ya binadamu,”alisema.
Aliongeza kuwa kutokuwa na uwiano mzuri wa kijinsia katika usaili katika elimu ya juu hasa katika sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati ni changamoto kubwa katika maendeleo ya elimu nchini.
“Maneno ya hekima ya Mwalimu, Mwanafalsafa, Mwafrika, mwenye asili ya iliyokuwa Gold Coast ambayo sasa ni Ghana, Mwanzilishi wa Chuo cha Achimota, marehemu James Emmanuel Kwegyr Aggrey, ni muhimu tuyazingatie," alisema Prof. Mwandosya.
Prof. Mwandosya alimnukuu Kwegyr Aggrey akisema, “njia ya uhakika ya kuwafanya watu wasiendelee ni kuwaelimisha wanaume tu na kupuuza elimu ya wanawake. Ukimuelimisha mwanaume una muelimisha yeye tu, lakini unapomuelisha mwanamke, una elimisha taifa lote.”
Aidha, Prof. Mwandosya ambaye alistaafu uwaziri akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais 2015, alisema anaaminia wizara yenye dhamana ya elimu itasaidia kurekebisha uwiano usioridhisha wa udahili wa wanafunzi na ajira za wanawake nyanja hizo.
Prof Mwandosya ambaye alishika nafasi ya pili nyuma ya Jakaya Kikwete katika mapendekezo ya mpeperusha bendera ya CCM kwa uchaguzi wa rais wa 2005, alikuwa mmoja wa makada wa kwanza wa chama hicho kuchukua fomu miaka 10 baadaye lakini akachujwa mapema.
Rais John Magufuli na Waziri wa Ujenzi katika utawala wa Jakaya Kikwete ndiye aliyepitishwa na mkutano mkuu wa CCM kabla ya kumshinda Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kupata asilimia 58.46 ya kura zote halali Oktoba 25, 2015.