Hatimaye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imemuachia kwa dhamana Mbunge wa Arusha Mjini kupitia CHADEMA, Godbless Lema baada ya kusota gerezani kwa zaidi ya miezi minne.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kupitia hoja za pande zote mbili zilizowasilishwa mahakamani hapo leo na kuamua kuzitupitilia mbali hoja za upande wa serikali za kumnyima Lema dhamana.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache kupita tangu mahakama rufaa kutupilia mbali rufaa ya jamhuri, huku ikishangazwa na hatua ya Lema kukosa dhama hadi wakati huo.
Mbunge huyo ameachiwa kwa dhamana yenye masharti ya wadhamini wawili wanaoaminika pamoja na kusaini bondi ya shilingi milioni 1 ambapo nje ya mahakama Lema ametoa shukrani zake kwa wote waliohusika na kubainisha kuwa serikali haikuwa na nia njema na yeye, lakini yeye amesimama na Mungu.
"Ninamshukuru sana mwenyezi Mungu, mke wangu, familia yangu, mawakili, viongozi wa chama na wananchi wote waliokuwa na mimi. Na kwa namna ya pekee mke wangu, kama ningepata nafasi ya kuoa tena, ningemuoa yeye. Pia mtoto wangu alifikia hatua akasema anatamani kufanya kosa ili aje alale na mimi gerezani, na akauliza ni kosa gani afanye ili aletwe gerezani" Amesema Lema
Kwa upande wa wakili wake Peter Kibatala amesema hatimaye kazi ya kwanza ya kuhakikisha Lema anapata dhamana imekamilika na kwamba sasa wanajipanga kwa ajili ya kushughulika na kesi ya msingi.
Kwa niaba ya CHADEMA, Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, amelaani nguvu iliyotumiwa na jeshi la polisi siku ya leo ya kuwapiga, kuwakamata na kuwatawanya wafuasi wa chama hicho waliofika mahakamani hapo kufuatilia kesi ya mbunge wao, huku akitangaza kuwa kwa leo hakutakuwa na tukio lolote la kisiasa mpaka watakapotangaziwa tena.