Bado Mienendo Yake Huielewi..Fanya Hivi Itakusaidia..!!!


WAKATI mwingine unaweza kujikuta njiapanda muda wa kutaka kuchukua maamuzi. Kila unachotaka kufanya unahisi kama unahitajika muda zaidi au uvumilivu zaidi. Katika maisha vitu vya namna hiyo huwa vinatokea!
Umeshawahi kuwa na mtu na kujikuta kama humuelewi hivi, halafu ukashindwa kujua ni uamuzi wa aina gani unafaa kuuchukua? Mtu ambaye unajitahidi kwa kila hali kumuonesha namna unavyompenda ila wapi! Anakuchukulia kawaida tu.

Wala haoneshi kuthamini wala kuheshimu upendo na mapenzi unayomuonesha. Ulishawahi kuwa naye? Au ndiyo huyo uliye naye? Hapa suala ni moja tu. Mueleze namna unavyojisikia kwa tabia yake.

Katika kumweleza huku unapaswa kutafuta siku ambayo ni tulivu, kwa maana kila mmoja asiwe na kazi kwa muda huo ili maongezi yenu yapate heshima inayostahili.

Tumia nafasi hiyo kuwasilisha yote ya moyoni unayojihisi juu ya tabia yake. Mwambie katika hali isiyokuwa ya kulaumu wala jazba. Eleza namna yote unavyoteswa na tabia yake isiyoonesha kukupenda wala kuuthamini upendo wako.

Baada ya kuhakikisha tayari anajua namna unavyojisikia, sikiliza atakachokisema. Kuwa makini kupima kauli zake na jinsi sura yake inavyomaanisha. Wengine wanaweza kukupa majibu mazuri huku sura yake ikiwa inaonesha dharau na kejeli. Haina maana!

Pima uzito wa maneno uliyomwambia na majibu atakayokupa. Ukiona vina uwiano na ni majibu mazuri, mpe nafasi nyingine hata kama hiyo ni mara ya pili anakukosea. Kuwa mvumilivu – bila uvumilivu hakuna mapenzi ya kweli. Uvumilivu ni mama wa mafanikio.

Baada ya kuwa tayari umemweleza jaribu kusahau makosa yake na ufungue ukurasa mwingine katika maisha yenu. Hapo haitakiwi tena kukumbushia makosa yaliyopita.

Hiyo itamnyima uhuru wa kufurahi kikamilifu na wewe pia kuna uwezekano mkubwa wa kuchochea migogoro isiyo ya lazima katika mapenzi yenu.

Maana unaweza kumkumbusha hili na yeye akakukumbusha lile. Na kila mmoja hapo akataka kumuona mwenzake ndiyo mkosaji zaidi. Mapenzi hayawezi kuwa mazuri kwa staili hiyo.

Baada ya kuwa mmemaliza tofauti zenu anza kuangalia mabadiliko chanya katika matendo yake. Ni kweli kabadilika? Au kilichobadilika ni staili tu ya kukunyima furaha ila balaa ni lile lile?

Kama alikuwa na skendo za vimada sasa huzisikii ila kila siku safari zisizokuwa na sababu na ukijaribu kuuliza anakwambia “kuna mambo naweka sawa”. Mambo gani? Hakwambii! Akirudi ‘break’ ya kwanza bafuni akaoge kwanza ndiyo arudi muongee.

Ikiwa unamfanyia mpenzi wako kila lililojema katika mahusiano na bado haoneshi kubadilika zaidi ya kukusema “we msemaji sana” au anatoa ahadi tu zisizotekelezeka, kuna jambo la kufanya.

Kaa naye kisha mueleze kwa mara ya mwisho juu ya tabia yake na umueleze hatua unayokwenda kuchukua kama asipobadilika. Mapenzi ni raha na amani. Kama mtu hakupi hayo basi hakufai.

Kwa nini kila siku mahusiano yako yawe ya masimango na majuto yasiyokwisha? Kila siku machozi yatoke kwako tu. Kwani wengine hawana wapenzi? Mbona hawalalami wala kuumizwa?

Unapaswa kujua kitu – anayekupenda atakujali na kukuthamini. Hata siku moja hatapenda kuona unahangaika na kulia kwa sababu yake. Ukiona mtu anaona unaumia na kuteseka kwa ajili yake halafu hana habari na wewe jua kuna namna. Siyo bure.

Kama hakuna ulichomkosea wala kumkera basi jua hana mapenzi na wewe. Iweje akupende halafu asijali chozi lako? Kivipi aseme anakuthamini wakati hajali maumivu yako? Kuwa makini. Kuwa makini zaidi!

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad