CCM Yawaonywa Wanaochafua Wenzao Mitandaoni


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar, imetishia kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi na wanachama wake wanaowachafua wenzao mitandaoni.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alionya wakati akizungumza na viogozi, watendaji na wafuasi wa CCM wa jimbo la Malindi alipokuwa katika ziara ya kuimarisha chama.

Alisema CCM kwa sasa inaandaa utaratibu kupitia vikao vyake vya kikanuni kuwaita baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kuhusika na tabia hizo ili kuwahoji na kuwapa nafasi ya kujitetea.

Aidha, vikao vinavyosimamia maadili baada ya hatua hiyo vitaweza kuchukua hatua za kinidhamu kwa watakaokutwa na hatia.
Vuai alisema kuwa ndani ya chama hicho kuna tatizo kwa baadhi ya viongozi kutokuwa wa kweli na waaminifu.

Aliongeza kuwa wapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakiwachafua viongozi wenzao kwa lengo la kuwawaharibia ili wasiweze kuendelea na nyadhifa zao.

Aidha, alionya kuwa chama kimekuwa na mwongozo katika mambo mbalimbali na kama kuna tatizo kanuni zinaelekeza kuwa linatakiwa kutatuliwa kupitia vikao.

Alieleza kuwa chama hicho kimekuwa kikitoa onyo na tahadhari za mara kwa mara ili watu wenye tabia hizo waache, lakini baadhi yao wamekuwa hawataki kubadilika, hali ambayo haiwezi kuvumiliwa.

Alikemea pia kitendo cha baadhi ya watu kutumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kuupotosha umma.

Aliwatuhumu CUF kuwa ndiyo wanaotumia mitandao hiyo kuupotosha umma kwa lengo la kukiangusha chama na serikali iliyopo madarakani.

Aliwataka wana CCM na wananchi kutobabaika na taarifa za uongo zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii dhidi ya CCM na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein.

“Serikali ya Zanzibar inaendelea kuongozwa na Rais wake Dk. Shein hadi mwaka 2020 utakapofanyika uchaguzi mwingine.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad