Dakika 180 za Makonda Kuwekwa Kitimoto Bungeni...!!!


HATIMAYE. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhojiwa kwa dakika 180 na kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutokana na kauli aliyoitoa  Februari mwaka huu inayodaiwa kudhalilisha hadhi ya mhimili huo wa Dola.

Makonda akiwa amevaa shati ya maua na suruali nyeusi aliwasili bungeni jana saa 4 asubuhi kuitikia  wito huo uliopitishwa na Bunge Februari 8 mwaka huu, ikiwa zimebaki siku saba tu kabla ya kuanza vikao vya Bunge la Bajeti.

Siku hiyo ya Februari 8, Bunge lilitumia dakika 45 kupitisha kwa kauli moja maazimio manne, likiwemo la kuitwa kwa Makonda na mkuu wa wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti kutokana na hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara akisema wateule hao wa Rais wametoa kauli zinazodhalilisha Bunge.

Wakati Makonda akisema wakati mwingine wabunge hulala bungeni kwa kukosa cha kuzungumza, Mnyeti aliandika katika ukurasa wake wa facebook kuwa wabunge ni wapuuzi kutokana na michango yao wakati walipohoji hatua ya Ma-DC na Ma-RC kutoa amri za kuwaweka ndani viongozi wa siasa.

Hata hivyo,  jana ilikuwa zamu ya mkuu huyo wa mkoa ambaye habari za ndani kutoka katika kamati hiyo zinaeleza kuwa alikiomba radhi chombo hicho cha kutunga sharia, baada ya kubanwa kwa maswali ambayo mengine alishindwa kuyajibu.

Kuhojiwa kwa mteule huyo wa Rais, huenda kukawatuliza baadhi ya wabunge walionukuliwa katika vyombo mbalimbali vya habari wakieleza kuwa iwapo Bunge lingeshindwa kumhoji mkuu huyo wa mkoa, moto ungewaka katika vikao vya Bunge la bajeti.

Hata hivyo, mteule huyo wa Rais bado anaweza kuzua gumzo bungeni kutokana na kauli na matukio mbalimbali yanayomhusu, likiwamo la kuvamia kituo cha Clouds ambalo aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Mnauye aliliundia tume iliyothibitisha Makonda kuvamia kituo hicho, ambayo hata hivyo yanatajwa kusababisha Nape kuvuliwa uwaziri.

Jingine ni utata wa elimu ya Makonda na madai ya kughushi na kutumia vyeti vya kidato cha nne vya mtu mwingine, ambayo mashtaka yake yamefikishwa Tume ya Maadili ya Viongozi na Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.

Akizungumza baada mahojiano hayo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, George Mkuchika alisema, “Leo (jana) tumekutana baada ya kuagizwa na Spika kwa mujibu wa kanuni za Bunge.  Kamati yetu hukutana pale tu inapoagizwa na Spika.”

“Spika aliagiza kamati yetu imuite makonda ili kumhoji kufuatia azimio la Bunge lililopitishwa Februari 8. Pamoja ana mambo mengine alitakiwa kufka mbele ya kamati kujibu tuhuma zinazomkabili.”

Mkuchika alisema kwa mujibu wa azimio hilo, Makonda alidaiwa kutoa kauli hiyo kupitia kituo cha Televisheni cha Clouds kwamba wabunge wanasinzia, jambo alilosema kuwa lilionekana kama dharau kwa Bunge.

“Napenda kutoa taarifa kuwa Makonda leo (jana) amekuja mbele ya kamati na ametupa ushirikiano mzuri, tumepokea maelezo yake na naweza kusema kuwa kamati imemaliza kazi yake iliyoagizwa,” alisema Mkuchika.

Alisema kwa mujibu wa taratibu na kanuni za chombo hicho cha kutunga sheria, kamati yake itakabidhi taarifa ya mahojiano hayo kwa Spika ambaye ndiye atakayeamua namna ya kutoa taarifa kuhusu kazi ya kamati hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad