Baada ya sekeseke la kupiga marufuku uuzaji na unywaji wa pombe kali viroba, wanywaji wa pombe za viroba mjini Dodoma wamebuni mbinu mpya ya kununua pombe hiyo iliyopigwa marufuku huku watumiaji hao wakiipa pombe hiyo jina la maziwa mgando au nzela.
Maeneo yanakopatikana viroba kwa wingi katika mji huo ni stendi ya Mkoa wa Dodoma na Jamatini ambapo wafanyabiashara humimina pombe hiyo katika chupa za konyagi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mtanzania kwa siku kadhaa mjini hapo, umeonyesha jinsi pombe hiyo inavyouzwa kwa shilingi 1,000 baada ya kujazwa kwenye chupa kubwa za konyagi.
Mmoja wa wauzaji wa pombe hiyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini, alisema biashara imekuwa ngumu na wao wanahitaji kupata fedha, hivyo wameamua kuja na njia mpya ya kuuza viroba hivyo. “Tutafanyaje ndugu yangu, maisha magumu, tumeweka viroba katika chupa kubwa za konyagi na tunawapimia kwa kutumia kakikombe kadogo kama ka kahawa kwa shilingi 1,000,” alisema mfanyabiashara huyo.
Aliongeza”Siwezi kuacha hii biashara, hapa ni stendi, wasafiri na makondakta wengi ndio wateja wetu na natengeneza fedha za kutosha, lakini sasa hivi nawauzia tu watu ninaowajua, kwani naogopa kukamatwa.”
Naye mmoja wa wanunuzi wa viroba hivyo, alisema baada ya Serikali kupiga marufuku uuzwaji wa viroba hivyo, wameamua kubadili mwelekeo wa kununua bidhaa hiyo ili kukwepa mkono wa Serikali.