Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye kwa sasa anaishi nje ya nchi, Willbrod Slaa amesema anajitathmini kwa kile kilichomfanya aondoke hapa nchini na familia yake kama hakipo aweze kurejea nyumbani.
Dkt. Slaa aliamua kuweka pembeni masuala ya siasa baada ya kutofautiana na chama chake juu ya masharti ya kumpokea aliyekuwa mgombea wa Urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Amesema kuwa kwa sasa amemaliza masomo yake na baada ya kutafakari na kujitathmini atarejea nyumbani muda wowote.
“Ni kweli nimemaliza masomo yangu, bado napima mazingira yaliyonifanya niondoke na familia yangu, baada ya hapo nitaangalia uwezekano wa kurejea nyumbani,”amesema Dkt. Slaa.
Aidha, kuhusu mwenendo mzima wa Serikali ya awamu ya Tano, amesema kuwa hakuna nchi hata moja ulimwenguni ambayo Rais wake atakubarika kwa asilimia mia moja, hivyo Rais Magufuli ameonyesha msimamo wa kusimamia kile anachokiamini
Hata hivyo, ameongeza kuwa kama wapinzani hawatakuja na ajenda makini na mkakati unaoweza kuwasaidia wananchi hapo walipo, basi upinzani unaweza kufutika mwaka 2020.
“Kama nilivyorejea mara kadhaa, upinzani makini utaingia Ikulu kwa ajenda mbadala. Ajenda makini yenye kuwalenga wananchi moja kwa moja katika kuwatoa kwenye kero zao mbalimbali.
“Hadi sasa ninachoona ni ‘kurukia’ kauli za JPM, lakini kauli si ajenda na hatupeani maksi kwa kuzungumzia usahihi wa lugha. Wako wanaotazama usahihi wa lugha na mahali pa kutazama usahihi huo. Kimsingi hayo ni masuala ya darasani au kwenye uandishi wa vitabu.
“Aidha kumtuhumu JPM kukiuka Katiba na sheria nayo haina tija. Wote wanaomtuhumu wanajua kuwa wakiambiwa waonyeshe kifungu mahususi alichokiuka yeye mwenyewe katika utendaji wake hawana majibu ya kuridhisha.
“Hivyo mimi sijaona mwenendo wa JPM unaosaidia kuingiza upinzani Ikulu. Isitoshe kama hawatakuja na ajenda makini na mkakati ulioandaliwa unaowatoa wananchi hapa walipo kwenda kwenye raha, upinzani unaweza kufutika kabla ya 2020,”alisema Dk. Slaa.
HUYO MSOMI AMEWEKA KANDO UCHAMA UKUTA nk.KWENYE UKWELI UONGO HAUNA NAFASI..MAY GOD BLESS MAGU n MACO..
ReplyDelete