RAIS Abdi El-Fattah Al-Sisi wa Misri amesema nchi yake imejitoa kwa hali na mali kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine za Afrika ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi kwa pamoja.
Alikuwa anazungumza na viongozi 37 wa vyombo vya habari kutoka nchi 27 za Afrika katika Ikulu ya mjini hapa, jana baada ya viongozi hao kuhudhuria mafunzo ya wiki mbili juu ya Mwelekeo wa Vyombo vya Habari Afrika kwa siku za usoni.
“Misri sasa inarudi tena barani Afrika na sera ya ushirikiano wa kuimarisha uchumi na ndugu zake wa nchi za Afrika ili kujiletea maendeleo,” alisisitiza.
Alisema Misri tayari inashirikiana na nchi mbalimbali barani katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na za kilimo, elimu na afya na kwamba sasa ipo haja ya kupanua zaidi kuimarisha ushirikiano huo katika miradi, uwekezaji na ujenzi wa miundombinu.
“Miradi ya kuunganisha barabara, ujenzi wa reli na usafiri wa majini ni muhimu katika kuimarisha usafirishaji wa bidhaa na mawasiliano na hivyo kukuza uchumi baina ya nchi,” alieleza.
Alikumbusha kuwa, kipindi cha kupigania uhuru kilishapita na kwamba sasa Afrika iko katika kipindi kingine cha kuimarisha uchumi wake na moja ya njia ya uhakika katika kutekeleza hilo ni kuboresha ushirikiano.
Alifafanua kwamba katika sera ya nchi yake ya kurejea Afrika, nchi yake haitafuti uongozi, bali ushirikiano wa kweli utakaoziongoza nchi za Afrika kuwa na lugha moja ya kushirikiana kwa kujiletea maendeleo.
“Tumerudi kwa ndugu zetu Afrika ili tushirikiane katika kujenga mataifa yetu kiuchumi,’’ alisisitiza Rais Al-Sisi.
Sera ya mambo ya nje ya Misri kwa muda mrefu imekuwa ikijielekeza kwa nchi za Mashariki ya mbali kutokana na ukaribu wa kijiografia na kiutamaduni, lakini sasa inajitahidi kurejea barani kwake Afrika kuimarisha ushirikiano.
Katika suala la vita dhidi ya ugaidi, Rais huyo alisema nchi yake kama ilivyo kwa mataifa mengine inapigana dhidi ya ugaidi na kwamba inatoa mafunzo kwa ajili ya watu wake pamoja na nchi nyingine barani Afrika ili kukabiliana na hali hiyo ya tishio la kiusalama.