UNAAMBIWA ukiona cha nini mwenzako anasema nitakipata lini, kwani baada ya Yanga kuamua kumtema kocha wao za zamani, Hans van der Pluijm, nyota ya Mholanzi huyo imezidi kung’aa na sasa ana ofa mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambazo zimekuwa zikimiminika kila kukicha.
Pluijm alibadilishwa kutoka kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo na kupewa cheo cha ukurugenzi wa benchi la ufundi muda mfupi baada ya waajiri wake, Yanga, kumwajiri kocha mwingine, George Lwandamina, aliyekuwa akiinoa timu ya Zanaco ya Zambia, lakini hakudumu muda mrefu, baadaye alitimuliwa kabisa kutokana na kile kilichodaiwa na uongozi kuwa ni ukosefu wa fedha.
DIMBA Jumatano limezungumza na Pluijm kuhusu mustakabali wake ambapo amesema anamshukuru Mungu kwa kuendelea kumpigania, kwani kwa sasa amekuwa akipata ofa mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambazo zinampa wakati mgumu wa kuamua aende wapi.
Alisema kwa sasa bado yupo Tanzania na wala hajaondoka kwenda kwao Ghana, ambapo amedai kuwa, anafanya mambo yake kimyakimya na yakishakaa sawa atawekakila kitu bayana ili Watanzania na wadau wanaomuunga mkono wafahamu.
“Kama kuna watu wanauliza, kama nipo Tanzania au nimeshakwenda Ghana waambie bado nipo hapa nchini, na kuhusu mustakabali wangu niseme kwamba siwezi kuzungumza mengi kwa sasa ila kwa kifupi nimepata ofa mbalimbali za hapa Tanzania na nje ya nchi.
“Kwa sasa nachukua muda kutafakari na kutuliza akili yangu halafu nitafanya maamuzi sahihi,” alisema kocha huyo, aliyeiletea heshima Yanga kutokana na kuwapa vikombe mbalimbali, huku pia akijenga mashikamano ndani ya timu.
Taarifa zaidi kutoka vyanzo mbalimbali zinadai kuwa, moja ya timu ambazo Pluijm anatajwa kujiunga nazo hapa nchini ni timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo kwa sasa ipo chini ya Jackson Mayanja.