ULAJI wa maboga ni muhimu lakini ni Watanzania wachache wanaojua faida ya boga na mbegu zake. Mbegu za maboga zimesheheni protini na madini kadhaa kama vile chuma, kopa, maginizia, manganizi na zinki, mbegu za maboga zinakuwa mbegu bora na muhimu kutafuna kila wakati baada ya kuzikaanga au zikiwa mbichi au kama zimepikwa na boga lenyewe kwani imethibitika pasipo na shaka kuwa mbegu za maboga zina faida lukuki kiafya na zina uwezo wa kukuepusha na magonjwa hatari zaidi ya 10.
KIBOFU CHA MKOJO
Mbegu za maboga zimekuwa zikitumika kuimarisha afya ya wanaume kutokana na kuwa na kiasi kingi sana cha madini aina ya Zinc ambayo ni muhimu sana kwa afya ya kibofu cha mkojo Urinery Bladder. Mbegu za maboga pamoja na mafuta yake, yote kwa pamoja hutoa kinga kwenye kibofu kupatwa na matatizo ya kiafya, yakiwemo yale ya saratani ya kibofu.
KINGA YA MWILI
Mbegu za maboga zenye kiasi kingi cha madini ya Zinc yana faida nyingi mwilini, ikiwemo kuimarisha kinga ya mwili, kuboresha ukuaji na uundaji wa chembechembe hai za mwili, kuboresha usingizi, kuboresha ladha mdomoni na harufu, huboresha afya ya macho na ngozi, hurekebisha kwenye damu sukari na huboresha nguvu za kiume pia huongeza uwezo wa kufikiri. Upungufu wa madini ya Zinc mwilini una uhusiano mkubwa sana na matatizo ya kuzaa watoto njiti, mwanamke au mwanaume kuota chunusi nyingi mwilini, watoto kuwa na uwezo mdogo wa kuelewa wanachofundishwa darasani kimasomo na matatizo mengine mengi ya kimwili na kiakili.
MAFUTA YA OMEGA -3
Omega-3 ni moja kati ya mafuta muhimu sana mwilini. Jamii ya karanga pamoja na mbegu za maboga ni miongoni mwa mbegu zenye kiasi kingi cha mafuta aina hii. Hivyo ulaji wa mbegu za maboga utakuwezesha kupata kirutubisho hiki muhimu katika mwili wako na kukupa faida za mafuta haya ambazo ni nyingi.
UGONJWA WA MOYO
Mbegu za maboga zina kiasi kingi cha madini aina ya maginizia Magnesium ambayo huboresha utendaji kazi wa viungo vya mwili. Huimarisha usukumaji wa damu kwenye moyo, huimarisha ukuaji wa mifupa na meno, huifanya mishipa ya damu kupitisha damu kwa urahisi na hufanya upatikanaji wa haja kubwa kuwa laini.
KINGA DHIDI YA SARATANI
Imethibitika kwamba watu ambao hula mlo wenye kiasi kingi cha mbegu za maboga wamegundulika kuwa na hatari ndogo sana ya kupatwa na saratani za tumbo, matiti, mapafu na kibofu, hivyo unapokula mbegu hizi husaidia mambo hayo na mengine mengi.
UGONJWA WA KISUKARI
Utafiti uliofanywa kwa kuwalisha wanyama mbegu za maboga, umeonesha kuwa ulaji wa mbegu za maboga, husaidia kurekebisha kiwango cha Insulin mwilini na hivyo kumuepusha mtu kupatwa na ugonjwa hatari wa kisukari.
MATATIZO YA UKOMO WA HEDHI
Mara nyingi akina mama watu wazima ambao wamefikia ukomo wa hedhi, hupatwa na matatizo mbalimbali yanayosababishwa na hali hiyo. Hata hivyo, wataalamu wamegundua kwamba ulaji wa mbegu umeonesha kuwa mbegu za maboga zina uwezo wa kurekebisha hali hiyo na kuondoa kabisa matatizo ya kiafya yatokanayo na ukomo wa hedhi.
AFYA YA MOYO NA MAINI
Mbegu za maboga, ambazo zina kiasi kingi cha mafuta mazuri, kamba lishe Fibre na virutubisho vinavyoimarisha
kinga ya mwili Antioxidants, zimeonekana kuwa bora pia kwa afya ya moyo na ini, huweza kumpatia mlaji kinga dhidi ya matatizo ya kiafya katika moyo na ini.
DAWA YA USINGIZI
Mbegu za maboga zimegundulika pia kuwa na kirutubisho kinachozalisha homoni za usingizi. Ulaji wa mbegu za maboga saa chache kabla ya kupanda kitandani, hasa ukila pamoja na tunda lolote, kunasaidia kupata usingizi mzuri mwororo.
DAWA YA UVIMBE
Wataalamu wamethibitisha kwamba mbegu za maboga zina mafuta yenye uwezo wa kutoa kinga dhidi ya magonjwa ya uvimbe Inflamatory Diseases sawa na dawa aina ya Indomethacin lakini mbegu hizi hazina madhara kama ilivyo kwa hiyo dawa, ndiyo maana tunahimiza kutumia mbegu za maboga ambazo huwa ni dawa asili.
JINSI YA KULA MBEGU ZA MABOGA
Ili kupata faida zake zote, zikiwemo zile za mafuta yake, inashauriwa kula mbegu hizo zikiwa kavu, bila kuzikaanga japokuwa zilizokaangwa bila kuunguzwa nazo siyo mbaya. USHAURI Hakikisha pia unapata mbegu zilizohifadhiwa vizuri ambazo hazijaoza wala kuwa na fangasi. Iwapo utapenda kuzikaanga, basi hakikisha unazikaanga kwa muda usiozidi dakika 15, unaweza pia kuongeza chumvi kidogo kupata ladha, lakini za kukaanga zitakuwa hazina mafuta mengi kama zile kavu.