Harmorapa: Mburudishaji mpya pendwa mwenye zali na kiki


TANGU juzi video na picha za Harmorapa zimekuwa zikisambaa mtandaoni ambazo zinamuonyesha msanii huyo akitimua mbio pindi alipoona kitendo cha kutishiwa na bastola kwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.



Hili la Harmorapa limechekesha wengi sana na hata kuwasahaulisha yale yaliyotokea siku hiyo. Ila sikujua kama jamaa ana mbio zile, wengine kwa sasa wamempa jina la utani ‘HarmoBolt’ wakitohoa jina la mwanariadha Usain Bolt kutoka Jamaica. Katika ‘kioja’ hiki naomba ni mzungumzie Harmorapa kwa haya machache pamoja na muziki wake tangu nilipoanza kumfuatilia.

Kwanza muziki ni tiba

Muziki una nguvu ya uponyaji amini usiamini, ndio tiba pekee duniani inayoweza kukutoa kutoka kwenye lindi la mawazo na maumivu angalau kwa masaa machache. Hayo ni maneno ya mwanamuziki nguli wa miondoko ya Rock na Blues, Elton John. Gwiji huyu kutoka ardhi ya Malkia Elizabeth (Uingereza) anajaribu kueleza ulimwengu umuhimu wa muziki katika maisha yetu pengine ni zaidi ya hata tiba.

Binafsi nasadiki juu ya hilo kwani Elton John ni mtu anayejua muziki haswaa. Ndiyo anajua, akiwa anashikilia tuzo tano za Grammy mkononi si wa kuchukulia poa. Twende mbele twende nyuma, ulishawahi kujiuliza ingekuwa vipi maisha bila muziki?. Swali hilo alishawahi kujiuliza Gwiji la muziki Remmy Ongala katika katika wimbo wake uitwao Muziki Asili Yake Wapi. Twende polepole vijana wengi wa Bongo Fleva, wengi mtakuwa hamhujui ila sio deni.

Lakini wimbo wa Belle 9 ‘Vitamini Music’ aliyompa shavu Joh Makini mtakuwa mnaujua. Wasanii hawa nao waliulezea muziki kama sehemu ya vitamini muhimu katika mwili ya binadamu. Tusimame hapo.

Harmorapa ndio doctor

Ni msanii aliyejitokeza hivi karibuni lakini amejichotea mashabiki lukuki akiwa na ngoma mbili tu mkononi. Rapa Kala Jeremah aliwahi kukiri kuwa Harmorapa amekuwa maarufu kuliko baadhi ya wasaniinwa hip hop wenye albamu mbili. Kwa vile muziki ni tiba kwa mujibu Elton John, basi wanaotoa huduma hiyo (wasanii) tunaweza kuwapachika jina la ‘doctor’. Kama ndivyo, basi Harmorapa ameweza kututibu kwa kipindi kifupi ambacho tumekuwa naye kwenye ‘game’ ya Bongo Fleva.

Utamu wa dawa yake unaanzia pale kwenye jina lake, sote tunajua jina hilo ni nakala (copy) ya jina la Harmonize msanii aliye chini ya lebo ya Diamond Platnumz ‘WCB’ inayofanya vizuri kwa sasa. Harmorapa kuweza kutengeneza jina la namna hii ndio inakuja maana halisi ya sanaa, ingawa kuna ambao wanaweza kusema jamaa anasafiria nyota ya mwenzake au anapenda ‘ganda la ndizi’.

Lakini kazi ya msanii ni nini kama si kutunga/kuumba na kuwasilisha katika hadhira?. Harmorapa kuwasilisha jina lake na ni moja ya kazi yake, au amekosea?. Tuachene na hilo.

Yeye kufanana na Harmonize ndio kumeleta ‘balaa’ lote hapa mjini kwa sasa na katika ‘game’. Kama isingekuwa hivyo sidhani kama leo hii ningeandika makala haya, tunazungumza na kuandika mengi kutokana na hilo.

Ametumia hiyo fursa ipasavyo na ameweza kuokota mashabiki kibao, kiufupi ametengeneza ‘attention’ kubwa kwenye ‘game’. Angalizo ni kwamba vitu nilivyoeleza kutoka kwake havina uhusiano wowote na muziki mzuri. Sijui kama unanielewa, narudia tena. Jina, muonekano na attention havimpi uhakika wa yeye kutengeneza muziki mzuri kama hatajitoa ipasavyo.

Diamond Platnumz alikaririwa akisema Harmorapa ameweza kutengeneza attention kwenye ‘game’ kinachotakiwa ni yeye kutengeneza muziki mzuri tu ili aweze kufanya biashara. Ndicho nilichokuwa nasisitiza hapo juu, bila hivyo anayofanya yote nje ya muziki hayatakuwa na maana.

Kwa sasa anatamba na wimbo utwao ‘Kiboko ya Mabishoo’ aliyompa shavu Juma Nature, bila shaka utafanya vizuri kutona na maudhui yake na vuguvungu lililopo kati yake na ‘dancer’ wa Diamond Platnumz, Mose Iyobo ila bado ni mapema kupigia mstari hilo. Lakini tumpe muda kijana.

Ajifunze, nafasi ipo wazi

Unakumbuka tukio la msanii PNC kushukiwa na mashabiki mitandao na hata wasanii wengine kumuimba kwenye nyimbo zao mara baada ya picha zake kusambaa mitandaoni akiwa amempigia magoti aliyekuwa meneja wake Ostaz Juma, bila shaka unakumbuka.

Lakini umejiuliza kwanini mashabiki hao hawakufanya hivyo kwa Harmorapa mara baada yeye kuonekana akimpigia magoti Alikiba wakati alipoenda kumpokea akitokea Afrika Kusini kuchukua tuzo yake ya MTV EMA. Ingawa haya ni matukio mawili tofauti ila kuna la kujifunza.

PNC hakustahili kufanya vile kutoka alikuwa ni msanii mkubwa na mwenye jina tayari, kiufupi yeye alikuwa mkubwa kuliko Ostaz Juma, si kwa maana mbaya. Lakini Harmorapa kwa Alikiba ni mdogo kwa kila kitu, yaani kiumri na hata kisanaa. Hivyo ni lazima ajishushe kwa watu waliyomtangulia ili waweze kumuelekeza baadhi ya mambo ya msingi, huku kunaitwa kujifunza. Kutokana bado yupo kwenye mchakato huu hakuna haja ya kumbeza na ndio maana mashabiki wakachukulia tukio hilo la kawaida.

Uzuri ni kwamba Harmorapa yeye binafsi analijua hilo, na kama sivyo, basi ‘management’ yake inahakakisha anafuata hilo. Kanuni ya mafanikio ni kukaa na wale waliokwisha kufanikiwa na kukueleza waliwezaje na pale waliposhindwa ili usije kupoteza muda hapo.

Kwa kulijua hilo si ajabu kuona Harmorapa akiwa katika picha tofauti na watu wenye heshima kubwa katika muziki wa Bongo Fleva kama Prof Jay, P-Funk na wengineo kibao. Juma lilopita P-Funk alikaririwa akisema Harmorapa anaweza kufika mbali endapo akitaka kujifunza zaidi. Kauli kama hii ni kama imemuwashia taa ya kijani na kazi ibaki kwake. Narudia tena, kauli hii imemuwashia taa ya kijani yeye tu ashindwe.

Maisha nje ya muziki

Kuna siku siku Harmorapa ‘alipost’ picha kwenye mitandao ya kijamii akiwa na fedha nyingi sana. Kitendo hicho kikanikumbusha michezo ya Floyd Mayweather na 50 Cent wakati walipokuwa wakirushiana maneno, yaani ‘beef’ ambapo kila mmoja alitakaa kuudhibitisha ulimwengu ana fedha nyingi kumzidi mwenzake.

Mchezo huu naona kwa hapa Bongo Dongo Janja na Young Killer wanajaribu kuucheza ila kwa upande wa kutambiana na magari. Raha na kusudi la michezo hii ni kuchangamsha ‘game’, kuna wakati muziki pekee hauwezi kufanya hivyo.

Nilipoona hiyo picha ya Harmorapa ninayokueleza nikajua wazi ameshajua mbinu moja wapo ya kuwachota mashabiki na kuwaleta katika muziki wake. Muda mwingine kile unachokifanya nje ya muziki wako kinasaidia kusukuma kazi yako kuwafikia watu wengi zaidi, na pengine nje muziki ndipo unapotakiwa kuweka nguvu zaidi. Ndiyo, nje ya studio unatakiwa kuwa mjanja zaidi. Hapa Bongo kuna wasanii wanajua kuimba pengine kumzidi Diamond Platnumz au wanapokuwa studio kiuimbaji wapo sawa lakini kinachowatofautisha kimafanikio ni yale wanayofanya nje ya muziki wao.

Harmorapa inabidi ajiongeze kwenye hili, asiishie kupiga picha na fedha nyingi kama nilivyotangulia kueleza. Kuna mambo ya makubwa na ya msingi anapaswa kufayafanyia kazi mara baada ya kutoka studio, jukwaani na pengine mbele ya kamera.

Kiki zake ugonjwa wetu

Chukua hii kwanza, nachoweza kukuambia kuna watu hawajui wimbo hata mmoja wa msanii Baba Levo lakini wanamtambua na kumpenda kutoka na vituko vyake.
Ule utani wake na wasanii wengine, kiki za hapa na pale yeye ni Shilole. Mtindo huo unamfanya kuendelea kuwepo kwenye ‘game’tu, bila shaka vitu vya namna mashabiki wanavipenda pia.

Nani kakuambia hawapendi, wee!!tazama ‘couple’ ya Harmonize na Jacqueline Wolper inavyokodolewa macho mitandaoni ingawa sote tunafahamu ni ‘kiki’ tu. Huu ni mchezo wa kuwavuta mashabiki karibu na kuwaweka tayari. Mchezo huu Harmorapa naye anajua kuucheza ipasavyo, na watu wanapenda na kufurahi kutokana yeye ni kijana mdogo lakini kiki zake za kibabe sana.

Ukipita katika mtandao wa Instagram lazima ukutane na picha zake akiwa na warembo fulani. Ndiyo, yeye na warembo. Kuanzia Gigy Money hadi Amber Lulu wote ni wake, sasa kwa nini watu wasimpende na kumfuatilia ikiwa anaukaribu na watu wenye ‘fun base’ kubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Na Harmorapa kujua mashabiki wanapenda mambo ya udaku kutoka kwa ‘mastaa’ wao, yeye anahakikisha juu chini kiki inapatikana maana ndio ugonjwa wetu.
Uzuri ni kwamba tukishaugua yeye mwenye anakuja kututibu kupitia muziki wake kama nilivyotangulia kueleza hapo awali. Nitamatishe kwa kumuhasa kuwa ajitahidi zaidi hapo kwa kuwa ‘game’ inaushindani mkubwa.

Angalizo

Mtaji mkubwa wa msanii ni kutoonekana mara kwa mara na kutozoeleka na watu ili anapoandaa ‘show’ watu wawe na kiu naye, hii pia itamfanya kupata ile mialiko maalumu (celebrity appearance) ambayo itaongeza dhamani yake.
Kwenye hili napata wasiwasi, Harmorapa amekuwa akionekana mara kwa mara, ni sawa yeye kuwepo pale kutokana Nape alikuwa Waziri wake kwa upande wa sanaa ila angetazama upepo uliyopo kwa sasa.

Hapa kulikuwa na makundi mawili yanavutana (conflict of interest) msanii usipokuwa makini unagawa mashabiki. Management yake itazame hili kwa jicho la tatu.

Na Peter Akaro
Author Professional: Journalist.
Contact: 0755 299596
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad