JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limejiweka kando kuhusu sakata la majina 65 ya watu waliyotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akiwatuhumu kujihusisha na dawa za kulevya.
Februari 2, mwaka huu, Makonda alitaja majina ya wasanii na maofisa wa Jeshi la Polisi wanaodaiwa kujihusisha na namna moja ama nyingine na dawa za kulevya na siku sita baadaye, alitaja orodha nyingine yenye majina 65 ya watuhumiwa wengine wa kadhia hiyo akiwagusa viongozi wa siasa, dini na wafanyabiashara.
Aliwataka kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na vyombo vya dola, wengi wao wakiripoti huku wachache wakikaidi agizo hilo la kudaiwa kukimbilia visiwani Zanzibar.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alipoulizwa kuhusu mwitikio wa wahusika kwenda polisi kama walivyotakiwa na Makonda, alisema suala hilo sasa haliko chini yake.
Alisema tayari walishakabidhi majina ya watuhumiwa kwenye ofisi ya Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya baada ya Rais John Magufuli kumteua Kamishna Mkuu, Rogers Sianga kuiongoza.
Kamishna Sirro alisema wanawashikiliwa watuhumiwa 105 wa dawa za kulevya ikiwamo bangi na pombe ya gongo. Alisema katika msako wao wamekamata dawa za kulevya kete 413 (bila kutaja ni aina gani), puli 50, misokoto ya bangi 86 na gongo lita 45.
Awamu ya tatu ya vita ya Makonda dhidi ya dawa za kulevya inahusisha majina 97 ya watu ambao hayakutajwa hadharani na Mkuu huyo wa Mkoa badala yake aliyakabidhi kwa Kamishna Sianga Februari 13 kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Katika hatua nyingine, Kamishna Sirro alisema jeshi hilo kupitia kikosi cha usalama barabarani, kwa siku tano kuanzia Februari limekusanya Sh. milioni 434 kutokana na makosa yanayofanywa na madereva wa vyombo vya moto.
WATOTO WAFUNZWA VITA
Aidha, Kamishna Sirro alitoa tahadhari kwa wazazi waliopotolewa na watoto wao kuwa wamebaini kuna kikundi ambacho huwachukua watoto hao na kwenda kufundisha mambo ya kivita.
Kamanda Sirro alisema wanaendelea kufanyia kazi taarifa za kuwapo kwa kikundi hicho ambacho alidai kinafundisha kareti na judo watoto kinyume cha sheria.
Alisema watu hao wenye nia ovu na nchi wamekuwa wakitumia baadhi ya makanisa na misikiti kwa ajili ya mafunzo hayo.
“Taarifa hizi tunaendelea kuzifanyia kazi ingawa wito wetu ni kwa wazazi ambao wamepotelewa na watoto wao, watoe taarifa polisi ili ufuatiliaji ufanyike mara moja," alisema.
Aliongeza kuwa kikosi chake kimeweka mitego maeneo yote ya ibada na kwingineko ili kuwasaka wahusika.
Kamanda Sirro alisema eneo la Kibiti mkoani Pwani limekithiri kwa uhalifu na vikosi vya Dar es Salaam vimejipanga ili wahalifu hao wasipate upenyo wa kuvuka mpaka kuingia Dar es Salaam.
"Tunawashikilia watuhumiwa wa uhalifu 20 ambao nane tuliwawekea mtego huko Kigamboni wakaingia, tulipata taarifa kutoka kwa wananchi juu ya wahalifu hawa, tunawahoji na wameanza kutaja matukio mengine ambayo wameshashiriki," alisema.
Kamishna Sirro alisema watuhumiwa waliobaki ambao ni 12 wanahusishwa na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha ambao walikamatwa maeneo tofauti ya jijini, miongoni mwao wakikutwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni hirizi.
Kamanda Sirro pia alisema wamefanikiwa kuzikamata pikipiki pamoja na magari matano yaliyokuwa yameibwa.
Kadhalika, alisema wamependekeza kuwa ili kukabiliana na wimbi la uporaji wa pikipiki na kupelekea wahusika kujeruhiwa na kuuawa, sheria itamke kuwa, biashara hiyo ifanyike mwisho saa 6:00 usiku.
“Nilitoa tamko kuwa waendeshaji wa pikipiki wafanye biashara hiyo mwisho saa 6:00 usiku, wapo ambao wanapiga kelele juu ya hili ila hawa wanaopiga kelele ni kwa sababu watoto wao hawajauawa,”alisema.