MAHAKAMA Kuu leo inataraji kutoa uamuzi wa maombi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema (Chadema), baada ya pingamizi la Jamhuri kuondolewa Mahakama ya Rufani Jumatatu.
Wakati Mahakama ya Rufani ikiridhia kurudishwa kwa shauri hilo Mahakama Kuu, mwenyekiti wa kopo la majaji watatu, Jaji Benard Luanda alisema walishangazwa na Mbunge huyo kushikiliwa kwa miezi minne bila sababu za msingi.
Lema anashikiliwa tangu Novemba 2, mwaka jana.
Jaji Luanda pia alihoji kama ofisi ya DPP ina wanasheria. Mbali na Luanda, jopo hilo linakamilishwa na Jaji Stella Mugasha na Jaji Kipenka Mussa.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi ndiye aliomba mahakama kuiondoa rufani hiyo kwa vile hawakuwa wamepeleka kusudio la kukata rufani kwa Msajili wa Mahakama ya Rufani, kosa ambalo waliligundua Ijumaa iliyopita baada ya saa za kazi za mahakama.
Rufani iliyoondolewa iliombwa na Njau, aliyepinga Jaji Dk. Modesta Opiyo wa Mahakama Kuu kumwongezea Lema muda wa siku 10 ili akate rufani ya kunyimwa dhamana nje ya muda.
Jaji Luanda aliwaagiza mawakili wa Lema kurudi Mahakama Kuu kuendelea na masuala ya dhamana.
DHAMIRA MBAYA
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari nje ya Mahakama ya Rufani Jumatatu kuwa Jamhuri ilikuwa ikifanya ucheleweshaji kwa dhamira mbaya dhidi ya Lema.
Alisema chama hicho kimesikitishwa kwani Lema yuko gerezani bila sababu za msingi, kitendo kilichowafanya waichukie mahakama kuona inapewa maelekezo na serikali, lakini kumbe ni "mchezo wa ofisi ya DPP."
“Leo Mahakama imetufariji sana na kuturudishia imani yetu kwao kuwa ni chombo kilichosimama kwa miguu yake kama mhimili wake na haipokei maagizo ya serikali."
Lema alianza kukaa mahabusu Novemba 2, mwaka jana, baada ya kukamatwa katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kusafirishwa kuletwa Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Arusha.
Novemba 8 alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, mbele ya Hakimu Desderi Kamugisha ambapo alisomewa shitaka la uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
Hakimu Kamugisha alikubali kutoa dhamana kwa Lema kwa madai kuwa sheria haizuii kutoa haki hiyo kwa mshtakiwa wa kesi ya uchochezi, lakini kabla ya kutamka masharti ya dhamana, Mawakili wa Serikali, Paul Kadushi na Materius Marandu walidai wana nia kukata rufani dhidi ya msimamo huo.
Kutokana na mawakili hao kusema hivyo, Hakimu aliamua kesi hiyo ibaki kama ilivyo, huku mtuhumiwa akisubiri maamuzi ya rufani ya Jamhuri katika Mahakama Kuu.
Jaji Dk. Opiyo alipotupa rufani ya Jamhuri na kumpa Lema siku 10 zaidi ili akate rufani ya kupinga kupewa dhamana bila masharti ya dhamana kwa kuwa hoja hizo hazikuwa na mashiko, mawakili wa serikali wakakata rufani Mahakama ya Rufani.
Tangu wakati huo Lema ameendelea kukaa mahabusu katika Gereza la Kisongo.