“Niko tayari kuachia uendeshaji wa kampuni iwapo kutakuwepo mtu mwingine mwenye uwezo zaidi ya mimi kuiendesha.”
Hii ni kauli ya Lee Jae-yong, bosi wa kampuni kubwa ya Samsung ya Korea ya Kusini, kauli ambayo amekuwa akiitoa mara kwa mara katika mahojiano na mamlaka za nchi hiyo kuhusu kuhusika kwake katika kashfa ya ufisadi inayomzunguka Rais wa nchi hiyo, Park Geun-hye.
Lee Jae-yong, anaendesha kampuni hiyo ya kielectroniki ya Samsung ambayo ni kubwa zaidi duniani kwa niaba ya baba yake ambaye ameathirika kiafya.
Lakini sasa hivi Lee anaweza kulazimika kuachia madaraka ya kampuni, kwani wiki iliyopita alikamatwa kwa tuhuma za rushwa, ufujaji fedha, kusema uongo, kuhamisha mali nje ya nchi kinyume na sheria na kuficha ushahidi ili kujinufaisha kijinai.
Kutiwa kwake mbaroni kulitokana na hatua ya mahakama moja kukubali ombi kutoka kwa timu maalumu ya waendesha mashitaka iliyoomba Lee akamatwe na kuwekwa kizuizini kungojea utayarishwaji wa mashitaka halisi yanayomkabili.
Mwezi uliopita wapelelezi walimtuhumu Lee kwa kutoa rushwa ya Dola za Kimarekani 36 milioni kwa taasisi zinazomhusisha Choi Soon-sil – mwanamke mmoja mwanandani wa Rais Park. Rais Park pia yuko chini ya uchunguzi wa mahakama ya katiba ya nchi hiyo.
Jitihada za awali za timu ya waendesha mashitaka kuomba hati ya kukamatwa kwa bosi wa Samsung ziligonga mwamba, ingawa baadaye mahakama ilibatilisha uamuzi wake, baada ya timu ya waendesha ilipotoa ushahidi wa ziada kuhusu uhusika wa Lee katika jinai zinazomkabili.
Hata hivyo mahakama ilikataa ombi jingine la kukamatwa kwa afisa mwingine mkuu wa kampuni hiyo, Park Sang-jin, kwa tuhuma kama hizo. Hati ya kukamatwa kwa Lee inawapa muda wa siku 20 kumshikilia ili kuendelea na uchunguzi.
Kutiwa mbaroni kwa Lee kunaonyesha kwamba kampuni ya Samsung haikuwa tu mhanga wa ulafi (extortion) kwa upande wa mamlaka za serikali. Wandesha mashitaka wanadai kwamba kutokana na malipo yale ya Dola 36 milioni, kampuni ya Samsung iliweza kupata msaada wa serikali, kupitia shirika lake kubwa zaidi la hifadhi ya jamii – (National Pension Service – NPS).
Msaada huo kutoka serikalini ilikuwa ni wa baraka zake kuunganisha makampuni mawili dada ya Samsung — yaani kampuni hodhi yake ya Cheil Industries na ile ya ukandarasi, Samsung C&T, zoezi liliofanyika Julai 2015.
Mwezi uliopita wandesha mashitaka walimfungulia mashitaka mkuu wa shirika la NPS kwa kosa la kutumia mamlaka vibaya. Walidai kwamba mkuu huyo aliamuru shirika kupiga kura yake kubariki muungano wa makampuni hayo mawili. Hata hivyo kampuni ya Samsung imekiri kwamba ilichotoa ni msaada wa mkopo tu na si rushwa.
Kutiwa mbaroni kwa Lee kunaashiria kwamba zile ‘njama’ zilizokuwapo baina ya mamlaka za serikali ya nchi hiyo na makundi ya makampuni makubwa ambayo ndiyo yalisukuma kukua kwa uchumi mkubwa wa nchi hiyo haziwezi tena kuendelea kuwapo.
Wachunguzi wengi wa mambo wanaona kwamba kwa muda mrefu mahakama za nchi hiyo zimekuwa zikisita kuwachukulia wamiliki wa makampuni hayo makubwa – ambayo kwa ujumla wake yanaitwa ‘chaebol.’
Inaelezwa kwamba baada ya awali mahakama kukataa kutoa hati ya kukamatwa kwa Lee mwezi uliopita, mitazamo miongoni mwa majaji ilianza kubadilika.
Mkuu wa kampuni ya Samsung, baba yake Lee Jae-yong ambaye yuko hospitali tangu 2014 alishahukumiwa mara mbili lakini kila mara alisamehewa adhabu na Rais aliyekuwapo madarakani. Hata hivyo mtoto wake bado hajafunguliwa mashitaka rasmi.
Aidha wanaharakati wa masuala ya sheria nchini humo wanasema kwamba wakuu wengine wa ‘chaebol’ – wakiwemo wale wa kampuni ya Hyundai, SK na Lotte wote wako mbioni kushughulikiwa.