Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki Dar es Salaam muhadhama Askofu Kardinal Polcarp Pengo, ametunukiwa cheti na Umoja wa Wanaume Wakatoliiki (Uwaka ) kwa kupanda Mlima Kilimanjaro.
Alikabidhiwa cheti hicho jana na Msaidizi wa Jimbo hilo Mhashamu Eusebius Nzigilwa.
Askofu Pengo hata hivyo alieleza kuwa hakufanikiwa kufika kwenye kilele cha mlima huo isipokuwa alithubutu pamoja na waumini wengine kadhaa, ambapo wachache miongoni mwao ndiyo walifanikiwa.
"Naamini kwamba hao wachache walifanikiwa kufika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro kwa sababu sisi tulianza nao hivyo walipata moyo, haitakiwi mwanaume uwe na moyo wa kukata tamaa," alisema Askofu Pengo huku akiwa amekaa kwenye kiti.
Pengo aliyasema hayo kwenye ibada ya maadhimisho ya Uwaka wakisheherekea msimamizi wao Mtakatifu Yosefu na Jubilei ya miaka 100 ya Upadre Tanzania.