MSHAMBULIAJI wa Simba, Laudit Mavugo ameibuka na kusema kuwa siri ya mafanikio ya kufumania nyavu hivi karibuni na kwenye mechi ya Yanga kunatokana na bibi yake aliyekuwa Bujumbura, Burundi kumsapoti na kumuombea kila siku.
Mavugo amekuwa na wakati mgumu wa kufumania nyavu tangu alipotua katika kikosi hicho cha Msimbazi, lakini siku za hivi karibuni ameonekana kuamka upya. Katika mchezo wa wikiendi iliyopita kati ya Yanga na Simba, Mavugo alifanikiwa kufunga bao lake la saba kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu wakati alipoiongoza Simba kupata ushindi wa mabao 2-1.
Akizungumza , Mavugo alisema amekuwa katika wakati mgumu wa kuweza kufunga lakini bibi yake aliyekuwa Burundi amekuwa akimuombea kwa muda mrefu hasa katika mechi ya Simba na Yanga ili aweze kufunga hivyo bao alilofunga anamzawadia yeye.
“Nimefurahi sana kuona nimefanikiwa kufunga, bao langu dhidi ya Yanga namzawadia bibi yangu aliyeko Bujumbura kwani amekuwa akiniombea nifunge hasa katika mechi hii dhidi ya Yanga.
“Mechi yetu na Yanga ilikuwa ngumu kwani kila upande ulikuwa ukihitaji kuibuka na ushindi, nakumbuka kabla ya mchezo bibi aliniambia ananiombea nifunge, hivyo bao hili yeye amehusika kwa kiasi kikubwa,” alisema Mavugo.