Imefichuka..Kutumbuliwa kwa Nape Nnauye Uwaziri Kumbe Bernad Membe Anahusika...!!!!


Duru za siasa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, zimeanza kutaja chanzo cha aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kupoteza wadhifa huo.

Vyanzo mbalimbali vinaonesha kuwa vumbi la Uchaguzi Mkuu la Mwaka 2015 bado linaendelea kutimka ndani ya CCM. Baada ya chama hicho kumfukuza uanachama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM, Sofia Simba, na wenyeviti watano wa CCM wa Mkoa katika Mkutano Mkuu wa Dharura mwezi uliopita mjini Dodoma, huku wengine wakipewa onyo, duru zinaonesha kuwa Nape Nnauye naye kawa mhanga.

Wakati wa mchakato wa kumpata mgombea wa CCM, Mbunge wa sasa wa Nzega (CCM), Hussein Bashe, alipata kumtuhumu Nape hadharani kuwa alikuwa akishirikiana na Mwenyekiti wa CCM (wakati huo), Jakaya Kikwete, kumbeba Bernard Membe.

Bashe alimtuhumu Nape kuwa katika kulipwa fadhila, Membe aliahidi kumwachia Jimbo la Mtama agombee, suala ambalo lilitokea Nape akagombea na kushinda. 

“Pamoja na kazi kubwa aliyofanya Nape kumnadi bwana mkubwa, bado wapo watu wamepenyeza maneno yaliyodhoofisha uhusiano wao. Mara kadhaa wamekuwa wakimwambia bwana mkubwa kuwa Nape ni wakala wa Membe ndani ya Serikali yake. Hili hakulipenda Mhe. Rais Magufuli, hivyo wakawa na mgogoro wa kimyakimya,” anasema mtoa habari wetu.

Vyanzo vya habari vinasema ushauri alioutoa Membe mara tu baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani na kupiga marufuku safari za nje, Rais Magufuli hakuupenda. “Tanzania si kisiwa,” alisema Membe wakati huo na kushauri Serikali isijitenge na jamii ya kimataifa kwa Rais na maafisa wa Serikali kutosafiri nje ya nchi.

Kinachodaiwa kuwa ni uhusiano wa Nape na Membe kiliongeza msukosuko baada ya Nape kupingana na kiongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam alipoamua kutangaza hadharani majina ya watu wanaotuhumiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya pale Nape aliposema, “Kutangaza majina ya watu bila ushahidi kunaweza kuharibu heshima na ‘brands’ za wasanii walizotumia nguvu na muda kuzijenga.”

Nape alitaka watuhumiwa wafikishwe mbele ya vyombo vya dola na wachunguzwe kisha watakaoonekana wana hatia wafikishwe mbele ya Mahakama kujibu mashitaka, ila si kutangazwa bila ushahidi kwani mbele ya safari inaweza kuthibitika hawauzi dawa za kulevya ikawa wameharibiwa heshima.

‘Kutia mafuta kwenye moto unaowaka’, Nape akaunda Kamati kumchunguza kiongozi kipenzi cha Mhe. Rais, pale kiongozi huyo alipovamia Kituo cha Radio na TV cha Clouds (CMG). Mkuu wa nchi alikwishasema ‘… chapa kazi. Usikwazwe na maneno ya mitandaoni.’ Kamati aliyoiteua Nape ikathibitisha kuwa hayakuwa maneno ya mitandaoni ni kweli kiongozi huyo alivamia Clouds, hili lilimkera mno Mhe. Rais akaona amtumbue,” kimesema chanzo chetu.

Gubu la kutoungwa mkono katika mchakato wa kisiasa linaonekana kuisumbua CCM kitambo sasa. Januari 30, 1984 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, alivuliwa madaraka mjini Dodoma, alipobainika kuwa alitaka katika uchaguzi wa mwaka 1985 aipe madaraka zaidi Zanzibar. Hii ya mwaka 1984 ilipewa jina maarufu kama ‘Kuchafuka kwa Hali ya Hewa Ndani ya CCM’.

Mwaka 1985, Maalim Seif Shariff Hamad alituhumiwa kumhujumu  Idris Abdul Wakil asipate ushindi wa kishindo Zanzibar, na pamoja na kumteua aendelee na Uwaziri Kiongozi wa Zanzibar, wawili hao waliendelea kuishi kwa kutoaminiana hadi Januari 26, 1988 wakati Abdul Wakil alipotengua uteuzi wa Maalim Seif na kumteua Dk. Omar Ali Juma.

Mgogoro uliendelea na ilipofika Mei 1988, Maalim Seif alijiondoa CCM. Seif aliondoka na akina Shaaban Mloo, Maulid Makame, Ali Haji Pandu na Hamad Rashid Mohamed. Baadaye kundi hili lilifungwa jela miezi 30 na liliachiwa baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi ambapo wote hawa walikwenda kuwa waanzilishi wa Chama cha Wananchi (CUF). 

Mwaka 1995, Augustino Mrema alijiondoa CCM baada ya kutofautiana na Serikali ya Alhaj Ali Hassan Mwinyi kuhusiana na kashfa ya mashamba ya mkonge Tanga, ambapo mfanyabiashara P. V. Chavda alipokuwa amepewa mashamba kinyume cha utaratibu. Mrema alijiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi ambapo alileta hamasa kubwa katika uchaguzi mkuu kwa kupata asilimia 27.7 ya kura zote.

Uchaguzi huo aliogombea na Benjamin Mkapa duru zinaonesha kuwa kama si nguvu ya Mwalimu Julius Nyerere, ilikuwa Mrema anaingia Ikulu. Ndani ya CCM yalibaki makovu na wengi walidhani CCM ingesambaratika baada ya wimbi hilo, ila baadaye ikajikusanya.

Februari 7, 2008, Edward Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu baada ya kuwapo taarifa za fitina kuwa alikuwa anajiandaa kugombea urais mwaka 2010. Ilielezwa kuwa Lowassa alikuwa na mkakati wa chini kwa chini kutenganisha kofia za Mwenyekiti wa CCM na urais, na kwamba Lowassa angetumia fursa hiyo kumwangusha Rais Kikwete.

Mgogoro huu wa chini kwa chini uliwagawa wafuasi wa viongozi hao ndani ya CCM, lakini ilipofika mwaka 2010 Lowassa hakujitokeza kugombea ubunge ikathibitika kuwa ulikuwa uvumi uliopenyezwa na wajanja waliokuwa wanajitafutia fedha.

Mwaka 2015, Rais Kikwete alipotangaza bayana kuwa Lowassa hawezi kuteuliwa kuwa mgombea ndani ya CCM na Chama kikampitisha Rais John Magufuli, Julai 30, mwaka huo Lowassa aliamua kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema. Uamuzi wa Lowassa ulileta changamoto kubwa, hali iliyopunguza kura za CCM na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii upinzani ukapata kura takribani asilimia 40.

Kutokana na hofu ya mgawanyiko uliotokea mwaka 2005, mwaka huu CCM imebadili kanuni yake baada ya kuwapo taarifa za chini kwa chini kuwa walikuwapo wana-CCM waliokuwa wanajipanga kugombea urais mwaka 2020, ambapo kwa sasa Rais aliyeko madarakani kwa CCM imepitishwa rasmi mwaka 2020 ndiye atakayekuwa mgombea wao.

“Mazingira haya unayoona hadi Rais anajiwekea kinga ya mwaka 2020 ndiyo yaliyomponza Nape. Wengi wanaamini Membe aliko huko nje ya ulingo wa siasa anafanya mazoezi ya kugombea urais. Kama vile hiyo haitoshi, wakubwa wameona wamwondoe hata Nape waliyedhani anawafikishia kila taarifa. Kwa hiyo, hata kama Nape asingekwaruzana na … bado wakati ungefika akaondolewa tu kwa nia ya kulinda siri za Serikali,” kimesema chanzo chetu.

Juhudi za JAMHURI kuthibitisha taarifa hizi kutoka kwa wasaidizi wa karibu wa Rais hazikuzaa matunda. Hata hivyo, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Humphrey Polepole, ameliambia JAMHURI: “Si kweli kabisa. Wanaosema hivyo, wapuuzwe. Kwanza Nape hakufukuzwa uwaziri, uwaziri wake haujatenguliwa, bali Rais amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri.”

Polepole amesema si dhambi wakati wa mchakato ndani ya chama kila mtu kuwa na mgombea anayempenda, ila baada ya mchakato kukamilika anayeteuliwa anakuwa mgombea wa wanachama wote. “Huo ndiyo utaratibu wa CCM. Baada ya mchakato tunavunja makundi. Hivyo aliyesema hivyo si mkweli. Apuuzwe.”

JAMHURI limemtafuta Nape kuzungumzia sakata la kufukuzwa kwake, akasema: “Kaka naomba mniache nipumzike kwa sasa. Maneno niliyokuwa nayo niliyasema siku hiyo mbele ya wanahabari. Nimesema bayana kuwa naunga mkono juhudi za Rais wangu kujenga nchi yetu. Sina kinyongo na Rais wangu. Nampongeza kwa uteuzi alioufanya na nitaendelea kuwa mwanachama mtiifu kwa nchi yangu na CCM.

“Nimesema mimi ni mbunge na namshukuru Mhe. Rais kwa kunipa nafasi ya kutumikia uwaziri. Wapo wabunge wengi, hawakuteuliwa kushika wadhifa huo, na hawakuhoji nilipoteuliwa mimi. Vivyo hivyo, umefika wakati wa Mtanzania mwingine kushika wadhifa huo, mimi sina kinyongo kabisa. Naunga mkono hatua hii. Niache nipumzike kidogo nitumikie wananchi wa jimbo langu la Mtama. Nawashukuru wanahabari na Watanzania kwa kuendelea kunipa moyo.”

Nape amekuwa ni miongoni mwa vijana wachache wa CCM ambao waliaminiwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, baada ya kutumikia nafasi ya ukuu wa Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, wilaya ambayo ni nyumbani kwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alipata nafasi kubwa.

Nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM aliipata baada ya kupitia katika tanuri kipindi hicho akiwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), baada ya kuwashambulia baadhi ya makada aliowatuhumu kuingia mkataba wa ujenzi wa jengo katika kiwanja cha Umoja huo kilichopo makutano ya barabara za Lumumba na Morogoro.

Nape alichukua nafasi baada ya kuachwa wazi na Mkuu wa Mkoa wa Tabora wa sasa, Aggrey Mwanri, ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Siha, mkoani Kilimanjaro. Ni kipindi ambacho Nape, pamoja na watumishi wengine wa Sekretarieti ya CCM, walikichukua chama kikiwa kimezongwa na tuhuma za ufisadi zilizokuwa zinawakabili wanachama wake.

Katika harakati za kukisafisha chama na kukirejesha kwenye mstari, alipata fursa ya kuzunguka sehemu kubwa ya nchi kukinadi CCM. Atakumbukwa kwa aina yake ya kuishambulia Serikali, hasa pale wananchi walipoonekana kutoa lawama kwa baadhi ya mawaziri.

Katika harakati hizo za kukijenga CCM, yaliibuka majina kama vile “mawaziri mizigo”, huku ujumbe huo ukiwa maarufu katika majukwaa ya siasa.

Ndani ya CCM, ambako leo Nape si miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu wala Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, nafasi ambazo alikuwa akiingia kwenye vikao kwa nafasi yake, leo hana nafasi hiyo tena.

Lakini mbali na kutokuwa kwenye nafasi hiyo tena, CCM kina jambo lolote la kujifunza kutoka kwa aliyekuwa Katibu wake wa Itikadi na Uenezi? Jibu ni rahisi sana, ndiyo. Hakuna anayeweza kubisha kwamba baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, CCM haikuwa inatamanika tena, wananchi wakapoteza matumaini.

Chama hicho kilipoteza mvuto zaidi baada ya kuingia mikononi mwa Wilson Mkama, msomi mzuri, ambaye alitarajiwa kuleta mageuzi makubwa ndani ya CCM, hasa kupitia mkakati wa kujivua gamba.

Chombo kilipoonekana kwenda mrama, Nape alichukua unahodha na kukiendesha kwa ustadi mkubwa. Mwenyekiti wa wakati huo na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, aliamua kumkumbuka rafiki yake wa muda mrefu, tangu wakiwa jeshini Abdulrahman Kinana, huku nafasi ya Itikadi na Uenezi akikabidhiwa kwa kijana mdogo wakati huo Nape akiwa na miaka 34 tu.

Hapo ndipo inapokuja historia ya kulala porini kwa siku zaidi ya 850, akijaribu kukijengea taswira mpya chama chake kwa wanachama. Jambo hilo amelisema hata baada ya kutishiwa bastola, akisema “Wakati ninahangaika na chama hiki, ninyi mlikuwa mnakunywa bia tu… nimezunguka nchi hii miezi 28, nikijenga chama changu CCM.”

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Fuateni sheria za nchi ns msipindishe majambo.mnaichezea nchi kama yenu na kuleta story zisizo na maana mkijuua Watanzania wengi hawazijui sheria zao. Makonda ana makosa ya jinai, kucheza na story ni janga na hatari kwa watanzania. Tatizo ni nini.?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad