HATIMAYE Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kueleza kiundani kile kilichowaponza baadhi ya makada wake waliotimuliwa mwishoni mwa wiki wakiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba na Mwenyekiti wake katika Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida.
Akizungumza kwenye kikao cha UWT mjini Dodoma jana, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye alimtuma mwakilishi, alisema wale waliotimuliwa baada ya kuvuliwa uanachama Jumamosi (Machi 11), walikutwa na makosa kadhaa yanayohusiana na maadili ikiwamo kuendelea kubaki kwenye makundi ya watu waliokuwa wakiwaunga mkono wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya chama chao hata baada ya kuteuliwa kwa Rais John Magufuli kupeperusha bendera yao.
Kinana ambaye katika mkutano huo wa UWT alikuwa akiwakilishwa na Katibu wa zamani wa NEC Idara ya Oganaizesheni ya CCM, Dk. Muhammed Seif Khatib, alisema kitendo hicho cha kutomuunga mkono Magufuli, ni baadhi ya makosa yaliyowaponza wahusika hadi wakavuliwa uanachama na kwamba hiyo ni ajali ya kisiasa kwa wahusika.
Wakati wa kuelekea chaguzi mbalimbali, kila mwana-CCM hutakiwa kuachana na kambi ya watu waliokuwa wakiwaunga mkono na kushirikiana kuhakikisha kuwa wagombea waliopitishwa kwenye vikao vyao halali ndiyo wanaungwa mkono ili mwishowe wafanye vizuri dhidi ya wapinzani.