Kada Chadema Mjini Moshi Alivyouawa Kinyama..!!!


MFANYABIASHARA wa Jiji la Dar es Salaam na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyewania ubunge wa viti maalumu wilayani Hai bila mafanikio katika uchaguzi mkuu uliopita, Anitha Kimario (44), ameuawa kinyama na maiti yake kukutwa kwenye shamba la miwa.

Awali, ilidaiwa kuwa Anitha alipotea katika mazingira ya kutatanisha kuanzia Jumatatu ya Februari 27 mwaka huu baada ya kuondoka nyumbani kwake Tarakea, Wilaya ya Rombo na kuaga kuwa anaelekea jijini Arusha kudai madeni yake yatokanayo na shughuli za kibiashara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa, alithibitisha kupokea taarifa za kuokotwa kwa mwili wa mfanyabiashara huyo ukiwa umevuliwa nguo zote na kutupwa katika matuta ya kuoteshea miwa karibu na Kiwanda cha Sukari cha TPC, Wilaya ya Moshi.

“Jana (juzi) saa 11:30 jioni, tulipokea taarifa kutoka uongozi wa Kiwanda cha TPC kwamba kuna mwili wa mwanamke umekutwa kwenye matuta ya kupandia miwa. Polisi walikwenda eneo la tukio na kuukuta mwili wake ukiwa umevuliwa nguo zote na kisha kufunikwa pembeni na udongo,” Alisema.

Kwa mujibu wa Mutafungwa, mwili wa mfanyabiashara huyo na kada wa Chadema, ambaye amegunduliwa kuwa ni mkazi wa Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam na Tarakea-Rombo mkoani, ulipatikana Machi 2 (juzi) ukiwa hauna majeraha yoyote kwa nje.

Alisema uchunguzi wa kina wa kitabibu utafanywa na madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa kushirikiana na Polisi ili kujua kiundani juu ya kile kilichotokea.

ILIVYOKUWA
Machi Mosi mwaka huu, makachero wa Polisi walilikuta gari la marehemu huyo aina ya Toyota RAV 4, lenye namba za usajili T 728 CEW, rangi nyekundu, likiwa imetelekezwa eneo la Bomambuzi, Manispaa ya Moshi, huku milango yake ikiwa imefunguliwa na funguo za gari zikiwa kwenye swichi.

Kamanda Mutafungwa alisema katika eneo la tukio, Polisi waliokota pochi ya mfanyabiashara huyo ikiwa na kadi yake ya uanachama wa Chadema, leseni ya gari, cheti cha uraia na kadi ya mpiga kura -- vyote vikimtambulisha kwa kina marehemu Anitha.

Alisema hadi sasa, mwili wa Anitha umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya KCMC na Polisi inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji hayo. Wanahojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi Mjini.

Akizungumzia msiba huo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, alisema amesikitishwa mno na mauaji ya mfanyabiashara huyo ambaye ni mwanachama wao na akaliomba jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini watu waliohusika na mauaji hayo ili sheria itwae mkondo wake.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad