Kama Kweli Una Ndoto za Kufanikiwa, Kaa Mbali na Hawa!


WIKI hii msomaji wangu nataka kuwazungumzia baadhi ya watu ambao wao wapowapo tu, wameridhika na maisha yao duni lakini haohao ndiyo wako mstari wa mbele kuwakatisha tamaa wenzao wanaopambana kutimiza ndoto zao.

Ukweli ni kwamba, maisha ya sasa yana changamoto nyingi, wanaoweza kuishi kwa furaha ni wale ambao kila siku wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii, lengo likiwa ni kuyaboresha maisha yao pamoja na wale wanaowategemea.

Achilia mbali hao ambao wanapambana kuyaboresha maisha yao, wapo ambao wamekuwa wakiota kuwa na mafanikio makubwa sana. Wamekuwa wakiumizwa vichwa vyao juu ya nini wafanye ili mwisho wa siku ndoto zao ziweze kuwa kweli.

Hawa ni wale wanaojua maana halisi ya maisha. Wanajua mafanikio ni kwa kila mtu na kwamba anayeishi ilimradi siku zinakwenda, hawezi kuwa na faida yoyote kwenye jamii anayoishi. Wenye mawazo hayo ndiyo wale ambao siku hadi siku huona mabadiliko katika maisha yao.

Wanaaga umaskini kwa kasi huku wakiona mwanga wa kutimiza ndoto zao. Mimi na wewe tunatakiwa kuwa hivyo.

Kuamini kwamba maisha ya kuwa na uhakika wa kula, kulala na kuvaa tu siyo tuliyopangiwa. Maisha sahihi tuliyopangiwa ni kuwa na uhakika wa kujipatia mahitaji hayo muhimu lakini pia kuwa na ziada ambayo itatufanya tuwasaidie wale ambao hawana uwezo.

Hapa nawazungumzia walemavu, watoto yatima na wazee. Hawa wanahitaji msaada wako, sasa kama utaridhika na maisha eti kwa kuwa umeweza kujikimu wewe na familia yako, utakuwa unakosea. Lakini sasa wakati wewe na mimi tukiwa kwenye jitihada za kutimiza ndoto zetu, wapo watu ambao wanashangaza sana.

Nawazungumzia wale ambao wamekuwa na tabia ya kuwakatisha tamaa wenzao
wenye uchu wa mafanikio. Watu hawa wapo huko mtaani. Unakuta wewe unakesha usiku na mchana, unapambana ili kutimiza ndoto zako, anatokea mtu kwa chuki zake anakuendea kwa mganga ili usifanikiwe au anakutia maneno ya kuvunja moyo ili usitimize malengo yako.

Watu hawa ni wabaya sana na unatakiwa kukaa nao mbali. Inawezekana kabisa wewe huna shida ya kufanikiwa, umeridhika na maisha yako duni unayoishi, kwa nini sasa uwe kizuizi kwa wengine wanaotaka kuzifanya ndoto zao ziwe kweli? Siku zote safari ya kuelekea kwenye mafanikio siyo ya ‘lami’, ina mashimo, milima na mabonde kiasi kwamba ili kufika kule unakotaka, inahitaji moyo na sapoti pia kutoka kwa watu wanaokuzunguka.

Ukiwa umezungukwa na watu wenye wivu, chuki na husuda, kufanikiwa kwako itakuwa ni kazi sana, waepuke hao! Ndiyo maana unashauriwa kuchagua marafiki, washauri
sahihi ambao unaamini ukiwashirikisha kwenye mawazo yako, wanaweza kukuunga mkono na kukupa sapoti inayostahili badala ya kukuvunja moyo.

Pointi ya msingi leo ni kwamba, mimi na wewe tunatakiwa kuhakikisha ndoto zetu zinatimia. Kikubwa ni kuzishughulisha akili zetu na kuweka malengo kwa kupita kule walikopita wale waliofanikiwa kabla yetu. Kingine ni kuhakikisha tunachagua watu sahihi wa kuwashirikisha mipango yetu ya kusaka mafanikio.

Siyo kila mtu atakuunga mkono, wengine watakukatisha tamaa, hiyo chukulia ni changamoto. Mwisho nishauri tu kwamba, kama wewe huna tamaa ya kufanikiwa, waache wenzako wanaojua lengo la kuletwa hapa duniani watimize ndoto zao.

Kama unajua huna uwezo wa kufanikiwa labda kutokana na sababu unazozijua, basi watie moyo wenzako kwani kufanikiwa kwao kunaweza kuwa na faida kwako.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad