Najua fika wapo ambao wamemaliza mwaka wa 2016 wakiwa hawajatimiza malengo yao ya kuwa miongoni mwa watu waliofanikiwa. Wewe unayesoma makala haya unaweza kuwa miongoni mwao, inaumiza sana!
Hata hivyo, huu siyo wakati wa kujilaumu bali unatakiwa kujipanga upya na kuanza tena pale ulipoishia, naamimi Mungu atakuwekea mkono na huenda mpaka mwaka unaisha utakuwa umefanikiwa.
Lakini sasa, nikupe angalizo tu kwamba, kama utakuwa ni mtu mwenye tabia hizi nitakazozieleza hapa chini, mafanikio utayasikia kwa wenzako tu.
Kutenda kabla ya kufikiri
Tabia ya kwanza ya watu wasioweza kufanikiwa kimaisha ni hii ya kutenda jambo kabla ya kufikiria. Watu wa aina hii huwa wepesi sana kununua vitu barabarani mara tu wanaposhawishiwa na macho au wauzaji.
Utakuta mtu bila hata kujiuliza faida za kitu hicho anaamua haraka kukipata. Ataamua kwa haraka kuoa, kuolewa, kukubali kujiingiza katika mapenzi na hata kufanya jambo lolote bila kujiuliza atanufaika vipi?
Kupenda kuzungumza zaidi ya kusikiliza
Watu ambao pia wako katika hatari ya kutofanikiwa ni wale ambao daima ni wazuri katika kuzungumza kuliko kusikiliza. Wao huwa ni wajuaji wa kila kitu, hawako tayari kupokea ushauri.
Siku zote wanapokuwa kwenye makundi ya watu, pengine wajuzi zaidi yao wao huwa hodari kujenga hoja kutetea mambo yao hata kama hayafai. Unaweza kumkuta mtu ni kiongozi wa ngazi za juu, amefanya kosa na watu wote wameona kuwa kakosea lakini mhusika hujiona si mkosaji.
Mtu anapokuwa muongeaji sana huwa mgumu kupokea ushauri wa yeyote, anachoamua yeye hukifanya kwa imani kuwa kinafaa. Ukiwa mtu mwenya tabia ya aina hii huwezi kufanikiwa kabisa katika maisha yako.
Watafiti wa masuala ya biashara ulimwenguni waliwahi kushauri kuwa, mipango mizuri ya kibiashara hutoka kwa watu maskini, ambao walisema hufikiri zaidi namna ya kujikomboa kuliko matajiri wanavyofikiri katika kujiendeleza, hivyo wakasema kama mtu anataka kufanikiwa kibiashara lazima asikilize mawazo ya maskini si kuwapuuza kwa kujiona ni bora zaidi yao.
Kukata tamaa mapema
Watu wanaotaka kufanikiwa huchukulia kushindwa kama hatua ya kuelekea kwenye mafanikio, lakini watu wasioweza kufanikiwa wanapojaribu mara moja au mbili kuvuka kikwazo fulani cha kimaisha na kushindwa, hukata tamaa na kutotaka kujaribu tena kusonga mbele.
Wenye tabia ya kushindwa kimaisha hawako tayari kudumu na jambo moja linaloonekana kushindikana kwao kwa muda mrefu. Akiona mwanamke ambaye ni mkorofi kidogo, haraka hukimbilia kumwacha na kutafuta mwingine, mara nyingi si watu wavumilivu.
Akijaribu biashara ya vitumbua kwa wiki moja na akaona havinunuliwi, anaanza kupika maandazi, wiki moja baadaye yuko kwenye mihogo, basi ilimradi kuhangaika kusikokuwa na tija katika maisha.
Asante sana������
ReplyDelete