Kukamatwa kwa Mhe. Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB) leo tarehe 6 Machi, 2017
Nimepokea taarifa muda mfupi uliyopita kuhusu kukamatwa kwa Mhe. Tundu Lissu (Mb) na Jeshi la Polisi leo asubuhi tarehe 6 Machi, 2017. Hii taarifa nimeithibitisha baada ya kuongea naye Mhe. Lissu kwa njia ya simu akiwa Central Polisi, Dar es Salaam.
Mhe. Lissu ambaye ni wakili mwenzangu, amekamatwa baada ya kesi dhidi yake, iliofungiliwa na Serekali baada ya kukamatwa kwake Bungeni mwezi uliyopita, kufutwa katika Mahakama ya Kisutu kwa maombi ya waendesha mashtaka. Alipokamatwa Mhe. Lissu alikua akilelekea kwenye kesi nyingine akiwa kama wakili mtetezi katika shauri hilo.
Tabia ya polisi ya kukamata watu baada ya kuachiwa na mahakama au kufutiwa kesi na waendesha mashtaka imeanza kuwa mazoea. Hii siyo mara ya kwanza imefanyika. Natoa rai kwa watumishi wa vyombo vya dola kwamba waheshimu haki za binadamu na waheshimu misingi ya sheria zetu. Kupindisha sheria ili kutimiza malengo ya watu fulani bila kuzingatia misingi ya haki itatupeleka pabaya kama nchi.
Kuna tetesi kwamba kukamatwa kwa Mhe. Lissu inahusiana na njama zinazofanyika na watu wasiojulikana kumzuwia kushiriki katika uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambayo inatarajiwa kufanyika tarehe 18 mwezi huu. Kama hizi tetesi zina ukweli wowote napenda kuweka wazi msimamo wangu kwamba uchaguzi wa TLS usiingiliwe na chombo chochote cha dola. Wanasheria waruhusiwe kuchaguwa Rais wanaomtaka.
Uchaguzi huu wa TLS umekuwa na msisimko wa kipekee kwasababu Wanasheria walio wengi wamechoka kuona haki za watanzania zikiminywa kwa matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Watanzania wanataka Nchi inayoheshimu utawala bora na utawala wa kisheria, na wanataka chama cha wanasheria ambalo lina nguvu ya kukemea pale ambapo haki haitendeki.
Kwasababu Jeshi la polisi hawajatangaza sababu ya kukamatwa kwa Mhe. Lissu ni vigumu kwa wakati huu kuongelea kilichosababisha akamtwe. Ni vema lakini kwamba Jeshi la Polisi litoe tamko mapema ili watanzania wafahamu ni kosa gani ambalo Mhe. Lissu ametuhumiwa kufanya. Kukaa kimya kwa Jeshi la Polisi itaendelea kujenga hisia kwamba kuna ukweli kwamba kuna njama ya kumzuwia Mhe. Lissu kushiriki katika uchaguzi wa TLS, jambo ambalo ni haki yake kama mwanachama aliyechujwa na kupitishwa kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa TLS.
Lawrence Masha
Machi 6, 2017