NAKIRI! Baada ya jina lake kuwemo katika orodha ya mastaa waliotuhumiwa kujihusisha na madawa ya kulevya, hatimaye msanii Lulu Abbas ‘Lulu Diva’ ameamua kuanika ukweli wake, kwa kukiri kuwa ni kweli ndiye aliyekuwa chanzo cha kukamatwa kwa mpiga picha Petit Man ambaye pia alitajwa kwenye listi hiyo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko juzikati, Lulu Diva alisema kukamatwa kwake kulitokana na picha ya unga mweupe aliyomtumia Petit Man, akimuuliza kilikuwa ni kitu gani, baada ya yeye kuwa ameupiga picha huko Afrika Kusini alikokwenda kikazi.
“Nilikuwa nimeenda Afrika Kusini kwa ajili ya kushuti video, sasa kutokana na gharama kubwa, nikawa nimeomba kwa wadau waniunganishe kwa Mbongo yeyote kule ili kusevu gharama, nikapewa dada mmoja hivi ambaye nilifikia kwake.
“Nikiwa kule nikawa simwelewi mwelewi hivi, kwani mara kwa mara walikuwa wanakuja polisi wanasachi na kuondoka, pia alikuwa anakuja na watu wengi wake kwa waume ambao sikujua wanafanya shughuli gani.
Sasa siku moja alikuja na watu wengi wakawa wamekaa wanaongea, walipoondoka wakaacha unga f’lani mezani. “Sijawahi kuuona hata mara moja, nikaupiga picha, sasa nikasema hebu nimtumie rafiki yangu Petit Man, nikamuuliza hiki ni kitu gani?” alisema binti huyo huku akisema picha hiyo ndiyo ambayo polisi waliikuta kwenye simu ya Petit Man na kumkamata.
“Baada ya kunitaja nilitafutwa siku mbili sikuwepo Dar maana nilivyorudi kutoka huko nilienda nyumbani Tanga kumuona mama yangu, nilivyorudi siku ya tatu usiku wa manane ndiyo nyumba ikazingirwa na polisi, nikachukuliwa na kupelekwa ‘Sentro’ ambapo nilikaa siku kadhaa kabla ya kupelekwa mahakamani.
“Kiukweli sijawahi kutumia au kubeba unga na siujui ila kiherehere changu cha kupiga picha na kuuliza kwa Petit ndicho kilichoniponza, bado naendelea kuripoti polisi kwa mwezi mara mbili kwa ajili ya kupimwa,” alisema Lulu Diva.
Lulu Diva ni miongoni mwa mastaa waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda katika orodha ya watuhumiwa wa madawa ya kulevya ambapo walikamatwa na kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuachiwa kwa dhamana kwa sharti la kuripoti kituo cha polisi Sentro mara mbili kwa mwezi.