Kimenukaaa...Madaktari Wacharuka, Wamtangaza DC Kilwa Kuwa Adui Yao Namba Moja....!!!!


Chama cha Madaktari (Mat) kimewataka viongozi wa serikali, hasa wakuu wa mikoa na wilaya kuacha kuwadhalilisha watumishi wa umma na kumtangaza mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai kuwa adui namba moja wa afya.

Mat pia imemtaka mkuu huyo wa wilaya kuomba radhi madaktari kutokana na kitendo chake cha kumuweka mbaroni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Dk Vitalis Katalyeba baada ya kumuona mkutanoni wakati aliagiza asimamishwe kazi kwa kutuhumiwa kuchelewesha gari la kumpeleka mgonjwa hospitali na kusababisha kifo chake.

Chama hicho pia kimewanyooshea kidole wateule wengine wawili wa Rais; mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Dk Rehema Nchimbi wa Mkoa wa Singida.

Rais wa chama hicho, Dk Obadia Nyongole alisema katika siku za hivi karibuni viongozi wengi wamejisahau na wanafanya vitendo vinavyokiuka haki na wajibu wa kada hiyo muhimu kwa afya za wananchi.

“Kitendo cha mkuu huyu wa wilaya (Ngubiagai) kinadhalilisha na kupunguza morali wa madaktari. Tuna shaka na uwezo wake,” alisema Dk Nyongole.

Kwa mtazamo wao, Mat inasema vitendo vya viongozi wa umma hasa wakuu wa wilaya au mikoa kuwanyanyasa madaktari na wafanyakazi vimekuwa vikiongezeka na vinafanywa ili kutafuta umaarufu wa kisiasa.

Alisema vitendo hivyo vinadhalilisha taaluma hiyo na kuwakatisha tamaa wanafunzi wanaosomea uganga waliopo vyuoni kwa sasa.

Ngubiagai aliagiza kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa Dk Katalyeba baada ya kubaini kuwa hakuwa na barua ya kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kama alivyoagiza awali.

Ngubiagai aliagiza Dk Katalyeba asimamishwe kazi baada ya kupokea malalamiko ya wananchi na wauguzi kuwa alichelewa kupeleka gari la wagonjwa kituo cha afya cha Tingi baada ya kupigiwa simu saa 4:00 asubuhi badala yake kulipeleka saa 10:00 jioni.

Muuguzi mmoja wa kituo hicho, ambaye alidai kumpigia simu Dk Katalyeba, alisema mganga huyo alimkatia simu na alipotuma gari mtoto huyo alikuwa ameshafariki, ndipo mkuu huyo wa wilaya alipoagiza asimamishwe kazi na kuchunguzwa, lakini mkurugenzi wa wilaya hakutekeleza maagizo hayo.

Akifafanua tukio lililotokea wilayani Kilwa, Dk Nyongole alisema aliyetakiwa kuipeleka barua hiyo kwa mkuu wa wilaya ni mkurugenzi na si mganga mkuu wa wilaya kama ambavyo Ngubiagai aliegemea wakati akifanya uamuzi aliouchukua mbele ya wafanyakazi wengine walio chini ya Dk Katalyeba.

“Inafahamika, mkurugenzi wa wilaya ndiye aliyepaswa kumpa mkuu wa wilaya barua ya kumsimamisha kazi daktari. Hii inatia shaka juu ya uweledi na uwezo wa Ngubiagai katika nafasi aliyopo. Tunaishauri mamlaka ya uteuzi kuangalia upya uteuzi wake,” alisema Dk Nyongole.

Mat inamtaka mkuu huyo wa wilaya kujitathmini kama anafaa kuendelea kuwahudumia Watanzania kwa nafasi hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad