Kimenukaaa...Umoja wa Mataifa Wajitosa Sakata la Kupotea kwa Ben Saanane,Taarifa Yao Yafunguka Mazito...!!!


Sakata la kupotea kwa mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben Saanane limechukua sura nyingine baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kusema upo tayari kutuma watu nchini kwa ajili ya uchunguzi.

Saanane, ambaye pia ni msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 18 mwaka jana na hadi sasa haijaeleweka kuwa alitekwa au kuuawa, ingawa Chadema imehusisha kutoweka kwake na taarifa ambayo Saanane aliitoa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu utata wa elimu ya baadhi ya viongozi.

Siku chache baada ya kupotea kwa Saanane, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliitaka Serikali kueleza kama inamshikilia kada huyo au ifanye uchunguzi wa kina kuhusu kupotea kwake.

Sanjari na hilo, Lissu aliitaka Serikali kufuatilia ujumbe wa vitisho ambao Saanane aliwahi kutumiwa kwenye simu yake ya mkononi na mtu ambaye bado hajafahamika.

Akisisitiza msimamo wa chama chake, Lissu alizitaka mamlaka zote husika na usalama wa raia ziseme hali halisi inayozingira sintofahamu ya mahali alipo, ikiwa yuko ndani ya nchi au nje, au hata kama amefariki na kuzikwa kwa kutotambuliwa.

Wakati utata huo ukiendelea, ofisi ya kamishna mkuu wa haki za binadamu duniani ya UN yenye makao yake makuu jijini Geneva, Uswisi, imesema iko tayari kutuma timu wa uchunguzi.

Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano uliotishwa na ofisi hiyo, Kanda ya Afrika uliohusisha nchi za Sudan, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Ethiopia, Djibouti na Tanzania.

Akizungumza na gazeti hili jana, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema suala hilo liliibuka baada ya wajumbe wa mkutano huo kutaka kujua undani wa sakata hilo, lakini hakukuwa na taarifa za kina.

“Wajumbe walionyesha kuguswa na suala la mtu kupotea katika mazingira ya utata na kutaka tuelezee kwa undani ilivyokuwa. Hatukuwa na taarifa za kina hivyo wakasema wako tayari kulifanyia kazi endapo tutatuma urgent alert,” taarifa ya dharura.

“Taarifa tutakayotuma ndiyo itakayowawezesha wao kutuma timu ya uchunguzi ije hapa baada ya hapo watajua ni kitu gani waseme kwa Serikali.”

Dk Bisimba alieleza kuwa bado taarifa hiyo haijaandikwa kutokana na kuwasubiri ndugu wa Saanane ambao wanatakiwa kutoa maelezo kwa kina.

“Tuliwaambia ndugu zake waje tupate maelezo yatakayotuwezesha kuandika hiyo urgent alert,  lakini bado hawajaja. Watakapofika tutaandika na kuituma ili uchunguzi ufanyike.”

Alipotafutwa kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa suala hilo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(DCI), Kamishna Robert Boaz alisema: “Nitafute Jumatatu kwa sasa nipo kwenye kikao.”


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad