SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya kuchapisha taarifa ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wenzake watatu, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna Msaidizi Salum Hamidu amedai mahakamani kuwa makala nzima iliyotolewa kwenye gazeti la Mawio ni ya uchochezi.
Pia, shahidi huyo alidai mahakamani jana katika kesi hiyo kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) na Hassan Nassoro Moyo ni miongoni mwa waliohojiwa katika makala inayodaiwa kuwa ya uchochezi.
Kamada Hamidu alitoa madai hayo wakati akihojiwa na mshtakiwa Lissu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Alidai kuwa katika malaka hiyo iliyochapishwa na gazeti la Mawio toleo la Januari 12-14, mwaka jana, Lissu alitajwa katika aya nane, Maalim Seif alitajwa katika aya 37, Dk. Alli Mohamed Shein alitajwa aya tatu na Moyo aya nne lakini hawapo kizimbani pamoja na washtakiwa wa kesi hiyo.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Lissu na shahidi:
Lissu: Shahidi, Rais wa Zanzibar ametajwa aya ngapi katika mahakama hiyo?
Shahidi: Ametajwa aya tatu.
Lissu: Maalim je?
Shahidi: Aya 37.
Lissu: Moyo naye ametajwa aya ngapi?
Shahidi: Moyo ametajwa aya nne.
Lissu: Je, makala nzima ni ya uchochezi?
Shahidi: Ndiyo.
Lissu: Kama ni hivyo mbona hapa kizimbani watu watatu hawajaungana na sisi kushtakiwa, Dk. Shein, Moyo na Maalim?
Shahidi: Mimi sihusiki na kuandaa mashtaka.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri April 3, mwaka huu.
Mbali na Lissu, washtakiwa wengine ni wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa magazeti, Ismail Mehboob.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, mwaka jana, Dar es Salaam, Lisu na wenzake walikula njama ya kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Pia Lissu na wenzake walidaiwa Januari 14, mwaka jana, Dar es Salaam, kwa nia ya kuleta chuki na uchochezi kati ya wananchi na mamlaka halali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walichapisha chapisho hilo lenye uchochezi.
Aidha, Lissu alidaiwa siku hiyo kinyume cha sheria na bila ya mamlaka waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.
Washtakiwa walikana mashtaka hayo na wako nje kwa dhamana.
Kesi hiyo iliposikilizwa mara ya mwisho, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimzuia shahidi huyo kuhojiwa na Lissu kuhusu Katiba ya Zanzibar na mamlaka ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya huko, Jecha Salum Jecha, kwa kuwa haina mamlaka ya kuzungumzia katiba hiyo.
Kadhalika mahakama hiyo ilisema haina mamlaka wala uhalali wa kuzungumzia majukumu ya Jecha na kwamba imekubali ombi la upande wa Jamhuri la kusitisha kumhoji shahidi wake kuhusu suala hilo.
Lissu alitaka kumhoji Hamidu, kuhusu Katiba ya Zanzibar.