Kusambaa kwa sauti iliyorekodiwa mazungumzo ya mwigizaji Steven Mengele ‘Steve Nyerere’ na mama wa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, Mariam Sepetu halijafutika, mengine yamefumka kwani baadhi ya wabunge waliotajwa kwenye sauti hiyo wamelimpua Steve. Mbali na wabunge kutajwa katika sauti hiyo iliyosambaa wiki iliyokatika, wasanii pia walitajwa ambao ni Khaleed Mohamed ‘TID’, Romeo George ‘Rommy Jones’ na Ahmed Hashim ‘Petit Man’.
Kwa upande wa wabunge ni Goodluck Millinga (CCM-Ulanga), Ahmed Shabiby (CCM-Gairo), Joseph Musukuma (CCMGeita Vijijini), Freeman Mbowe (Chadema-Hai) na Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo, Kigoma Mjini).
Steve pia aliwataja mawaziri wawili. Steve alisikika akiwataja wabunge hao akimwambia mama Wema kuwa, aliwafuata bungeni mjini Dodoma, Februari 6, mwaka huu ili wamsaidie bintiye aliposhakiliwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Dar ‘Sentro’ kwa madai ya kujihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya, ikiwemo kukutwa na bangi.
STEVE AOMBA RADHI WOTE
Hata hivyo, baada ya sauti hiyo kusambaa mitandaoni Februari 23, mwaka huu na kuwa gumzo, Jumamosi iliyopita, Steve alifanya mkutano na waandishi wa habari katika Jengo la Millennium Tower, Kijitonyama na kuwaomba radhi wote aliowataja huku akikiri sauti ni yake na kwamba, hakuzungumza nao kama ‘alivyomwongopea’ mama Wema bali aliwataja katika hali ya kudumisha ukaribu wake na familia ya mama huyo.
UWAZI NA WABUNGE
Baada ya mkutano huo, Uwazi liliwatafuta wabunge hao, kasoro Mbowe hakupokea simu, na waliopatikana walikuwa na haya ya kusema: SHABIBY: “Steve Nyerere namfahamu. Lakini sina ukaribu naye. Niliwahi kukutana naye muda mrefu kwenye hoteli yangu ya Moleno, Dodoma.
“Nakumbuka alikuja na mwanamuziki Ray C (Rehema Chalamila), lakini baada ya hapo sijawahi kuonana naye popote maana hata baada ya kukutana naye sikuwahi kuwasiliana naye. “Kuhusu kunihusisha mimi katika sakata la Wema, yale mazungumzo nimeyasikia vizuri. Si kweli alichokisema eti alikuja kukutana na Musukuma kwenye hoteli yangu na mimi nikiwepo. Ni uongo mtupu.
“Sijaonana na Steve Nyerere katika siku za hivi karibuni na sijazungumza naye lolote lile hata kwa njia ya simu,” alisema Shabiby.
MILLI NGA: “Ninafahamu kila kitu kinachoendelea, maana Steve Nyerere ni mtu ambaye tunakutana mara kwa mara, ukizingatia ni kada mwenzangu kwenye Chama Cha Mapinduzi. Kuhusu yeye kunishawishi mimi kumtetea Wema bungeni, jambo kama hilo halipo maana sikuwahi kukutana naye kabla ya mimi kuzungumza bungeni. “Ila baada ya bunge, jioni nilikutana naye, akaniambia kuwa, nilichokiongea ni kama nilitazama kilichokuwa moyoni mwake.
Hata hivyo, nimemsamehe maana ameomba radhi kwenye mkutano na waandishi wa habari!”
ZITTO: “Mimi siwezi kusemea jambo hilo maana mimi kwangu halina maana yoyote.”
MUSUKUMA: “Nisikilize vizuri mwandishi, mimi Steve Nyerere hana mchango wowote kwenye maisha yangu. Mimi ni Mbunge wa Geita Vijijini na sifanyi kazi yangu ya ubunge kwa kushawishiwa na mtu. “Steve Nyerere anaweza kunishawishi mimi kwa kipi? Ngoja nikwambie kitu, kinachoendelea ni kiki ya Steve Nyerere na watu wake maana kama umesikia ile ‘place’ na waandishi aliyoitisha, anasema Makonda ni rafiki yake, sasa unaweza kupima kinachoendelea hapo.”
MUSUKUMA AKATAA RADHI YA STEVE
Alipoulizwa kuhusu radhi aliyoiomba Steve Nyerere kwa wote aliowataja yeye ameipokeaje, alisema: “Kama ameomba radhi basi amewaomba wananchi
wangu wa Geita waliyoniweka kwenye nafasi yangu kwa lengo la kuwatetea wananchi na si kufanya kazi kwa ushawishi wa mtu.”
TID KWENDA KORTINI? Taarifa zaidi zilisema kuwa, Mbongo Fleva, TID anajipanga kumfikisha Steve kortini baada ya sauti yake kumtaja akisema anamchukia sana yeye huku pia kukiwa na habari kwamba, baadhi ya wanasheria jijini hapa wamepanga kujitokeza kwa waliotajwa ili kuangalia uwezekano wa kumfungulia kesi mama Wema ambaye anatajwa na Steve mwenyewe kuwa, ndiye aliyemrekodi.