Siku chache baada ya kuibuka hofu kuwapo kwa uwezekano wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuikatia nishati hiyo Zanzibar kutokana na deni inalodaiwa, visiwa hivyo vimepata matumaini ya kuwa na umeme wake wa uhakika.
Matumaini ya Zanzibar kuondokana na tatizo la umeme wa kutegemea sehemu moja yameanza kuonekana baada ya utafiti wa nishati mbadala unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kuonyesha uwezekano wa rasilimali hiyo kupatikana bila ya matatizo visiwani hapa.
Akizungumza katika ziara iliyofanyika jana kwenye vituo vya utafiti wa uzalishaji umeme wa upepo na nishati ya jua mikoa ya Zanzibar, Meneja wa mradi huo, Munir Shirazi Hassan alisema utafiti ulioanza mwaka 2016 kwa ufadhili wa EU unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili na kufuatiwa na ushauri yakinifu kutoka kwa wataalamu.
“Tunasubiri kwa hamu huduma hii ianze kutumika, tunadhani kufanikiwa kwake kutasaidia kushuka kiwango cha matumizi ya umeme kutoka Tanesco kwa zaidi ya asilimia 50 ili kuondokana na deni la matumizi ya kila mwezi.”
Ofisa mawasiliano kutoka Kampuni ya Ubelgiji, Sebastian Sanga alisema kukamilika kwa mradi huo kutaiondolea Zanzibar adha ya kutegemea umeme kutoka sehemu moja.