Kutana na Watu Wanaosherekea Siku ya Kucheza Kwenye Matope,...!!!


NI moja ya wiki za furaha nchini Brazil, ambako maelfu kama si mamia ya wananchi na wageni hujimwaga mitaani kusherehekea sikukuu kubwa zaidi nchini humo ya Karnivali.

Sikukuu hiyo haijali masikini wala matajiri, nyota wala watu wa kawaida kwani watu wa rika na matabaka tofauti hujimwaga mitaani kusherehekea kwa siku tano.

Mwaka huu ilianza Jumamosi iliyopita, ambapo mitaa ilipambwa na washerehekeaji hao wakiwa na mavazi ya mitindo mbalimbali huku wakicheza na kunywa.

Lakini wakati miji mbalimbali mikubwa ikiwamo Rio de Janeiro hali ikiwa hivyo, mamia ya washerehekeaji walimiminika katika mji wa Paraty wa ufukweni kuogelea matopeni wakati wa maadhimisho hayo.

Kwa mji huo mdogo, kuvaa mavazi ya thamani, manyoya, ngozi na kila aina ya mapambo ambayo huitambulisha Sikukuu ya Karnivali nchini Brazil hayana nafasi.

Watu katika mavazi ya kuogelea topeni katika mji huo, huonekana kama ilivyokuwa Jumamosi iliyopita wakijitupa katika mabwawa ya tope jeusi ndii, lenya utajiri wa madini kwa ajili ya sherehe hizo.

Sherehe hizo za tope zinajulikana kama 'Bloco da Lama', maneno ya Kireno yenye maana ya Sherehe za Tope za Mtaani.'

Simulizi zinasema 'Bloco' ilianzia mwaka 1986 wakati vijana wa mitaani walipokuwa katika matembezi ndani ya msitu wa karibu. Wakiwa humo walijikuta wakiwa ‘chakula cha mbu’ na hivyo wakalazimika kukimbilia katika tope kuogelea mwili mzima wakiwa na imani litasaidia kuwazuia mbu.

Katika hali hiyo mithili ya vibwengo walijikuta wakitokea mjini Paraty na kuzua mshangao mkubwa kwa wakazi na walioshuhudia huku baadhi wakikimbia.

Kwa vile lilionekana la kuvutia, kila mwaka likawa likifanyika kukumbuka tukio hilo na washerehekeaji wakawa wakiongezeka mwaka hadi mwaka hadi walipopigwa marufuku kuranda randa mjini.

Walizuiwa kuingia mjini baada ya wauza duka kulalamika kwamba kuta zao zilichakazwa na uchafu wao, ambao ulikuwa mgumu kufutika.

Hivyo, katika kusherehekea badala yake, washerehekeaji walikula, kunywa na kucheza ufukweni wakichafuka kwa matope huku wakiyarudi kama kawaida magoma ya Kibrazil.

Paraty ni mji mdogo wa ulio katika jimbo la Costa Verde, ukiwa baina ya majiji makubwa ya Rio de Janeiro na São Paulo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad