Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema anashukuru mazingira ya sasa yameuamsha umma kujua haki zao.
Lissu pia amesema mazingira magumu kisiasa yaliyowekwa na utawala, yamewafanya wapinzani kupata fursa za kujiimarisha.
Mbunge huyo wa Singida Mashariki alikuwa akizungumza na waandishi wa gazeti hili alipofanya ziara juzi katika ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL) inayozalisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen.
“Ni kama tuko njiapanda kwa sababu mahali tulipofika ni ama tusimame kama taifa au mwananchi mmojammoja tupinge hali hii,” alisema Lissu.
Alidai kuwa nchi imekuwa ikiendeshwa kibabe na kutofuata demokrasia, hali aliyosema inawafanya wananchi wasipate haki zao, uhuru wao wa kuzungumza, uhuru wa habari na haki za msingi.
“Si makundi ya kijamii, vyama vya siasa, vya wafanyakazi, vya kijamii, wasanii na hata nyinyi media tusimame kutengeneza harakati za kupambana na giza nene,” alisema Lissu.
Alisema nchi haiwezi kusonga mbele kama hakuna vyombo huru vya habari, kama wanasheria watajificha na kama makundi mengine ya kitaaluma yatakaa kimya.
Lissu alisema kwa sasa vyama vya siasa vimezuiwa kufanya mikutano ya hadhara, lakini hilo halijawafanya wakate tamaa wala kukubaliana na hilo.
“Katika historia ya mapambano, vyama vya siasa, taasisi za dini, vyombo vya habari, vyama vya kiraia. Wasanii kihistoria na si akina Ney wa Mitego wamechangia sana tangu miaka ya 1950 wamechangia kupatikana uhuru.”
“Nyie waandishi wa habari na vyombo vyenu vina nafasi kubwa kama wanasheria tu. Kusipokuwa na independent press (uhuru wa vyombo vya habari) mapambano yanakuwa magumu. Kama wanasheria wanajifungia kwenye chemba zao mapambano yanakuwa magumu hasa kwa wanaoteswa lakini ili iwezekane tunahitaji nguvu ya kila mtu,” alisema mbunge huyo ambaye mara kwa mara amekuwa akikamatwa na jeshi la polisi akidaiwa kutoa kauli za uchochezi.
“Si sahihi kusema kuwa tumekubaliana na hali hii,” alisema Lissu alipoulizwa kama wamekubaliana na uamuzi wa Serikali kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa.
“Hatujapotea, kama unaona adui amejipanga una-retreat (unarudi nyuma kujipanga). Kwenye vita kuna tactical retreat (kurudi nyuma kimkakati) ili kujipanga upya.
“Tunakabiliana na hali ambayo hatujawahi kukabiliana nayo tangu mwaka 1992. Awali, wapinzani tulidharaulika. Walisema hawana uwezo wa kufanya mikutano, lakini sasa mikutano ya hadhara ni hatari kwa walioko madarakani.”
Alisema kuonyesha kuwa mikutano ya wapinzani sasa inawatisha watawala, mwaka jana jeshi polisi lilifanya mazoezi hadharani likionyesha magari ya deraya na silaha, tofauti na hali ilivyokuwa zamani kuwa kazi ya chombo hicho kubakia kuwa ni kupambania nchi.
Alisema ndio maana waliamua kutotekeleza azma yao ya Ukuta ya kuandamana na kuendesha mikutano nchi nzima.
“Kwa hiyo ilikuwa ni kuamua; twende tukauawe au turudi tukafikirie upya. Ilikuwa ni uamuzi sahihi (wa kutofanya mikutano),” alisema Lissu.
Lissu alisema kuwa walidokezwa na kiongozi mmoja kuwa hali ingekuwa mbaya kama wangetekeleza azma yao ya kuandamana.
Chadema ilitangaza kuwa ingeanzisha maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia Agosti 31 mwaka jana kuendesha operesheni waliyoiita Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
Tangazo la kampeni hiyo lilifuatiwa na Jeshi la Polisi kuonya dhidi ya mpango huo na baadaye askari wake kuanza mazoezi ya mitaani, wakionyesha silaha mbalimbali za kukabiliana na waandamanaji.
Baadaye Chadema ilisitisha mpango huo ikisema imetoa nafasi kwa viongozi wa dini kuzungumza na Serikali.
“Ukuta haukuishia palepale. Ukitaka kujua tulikuwa sahihi kutofanya maandamano mwaka jana Septemba na ukitaka kujua ni jinsi wapinzani wa (Rais John) Magufuli walivyoongezeka. wameongezeka kwelikweli,” alisema Lissu.
“Leo upinzani umetapakaa kila mahali. Vile vigelegele vimepotea. Hakuna makundi yanayojitokeza na kuunga mkono yanayofanywa na Serikali. Kwa sisi, kutochukua uamuzi mwaka jana leo kila mtu anajua.
“Sasa kuna upinzani ndani ya chama tawala na ndani ya Bunge ni mkubwa zaidi. Pamoja na giza nene tunalokabiliana nalo, lakini kuna weupe mwingi. Upinzani umekuwa more generalized (wa sehemu tofauti). Upinzani unakwenda nje ya vyama vya siasa. Marufuku ya mikutano sasa haina maana tena.”
Aliongeza kuwa hata uamuzi wa kutorusha matangazo ya moja kwa moja ya baadhi ya shughuli za Bunge, haujafanikiwa kuzima upinzani.
“Nilisema mwaka juzi vigelegele havitadumu, ukiangalia kwenye vyombo vya habari hilo linajidhihirisha,” alisema.
Kubadili mbinu
Lissu alisema kuzuiwa kwa mikutano kumekuwa fursa nyingine ya kujiimarisha ambayo hawakuijua awali.
“Chadema ilikuwa chama cha mikutano ya hadhara kwa hiyo vikao vya ndani havikuwa muhimu na hivyo internal structures hazikuwa nzuri,” alisema Lissu.
“Tumebadilisha mapambano na sasa tunafanya mikutano ya ndani. Mikutano ya ndani imekuwa na mahudhurio makubwa. Imetusaidia kuimarisha internal structures.”
Tangu mwaka jana, viongozi wa juu wa Chadema pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu wamekuwa wakizunguka kwenye kanda za chama hicho, kufanya mikutano ya ndani na baadaye kusimika viongozi.
Alisema marufuku hiyo ya mikutano ya hadhara haitadumu kwa sababu ya shughuli za kisiasa zinazokuja, kama uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Nguvu ya Lowassa
Lissu pia alizungumzia ujio wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa akisema uliongeza nguvu muungano wa upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Ukizungumzia uchaguzi tu; umpende au umchukie, umtukane au umshangilie, huyu mtu anapendwa. Kura milioni 6.07?” alisema.
“Ukichanganya kura walizopata wagombea wa upinzani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995, Lowassa amepata kura nyingi kuliko wote. Ni kiongozi wa kihistoria. Pamoja na uzee wake, Watanzania hawa na matusi yote waliyomtukana bado ana nguvu kiasi hicho. Hali yake si nzuri sana, lakini ana nguvu kiasi hicho.”
Lowassa alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, lakini alijiuzulu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura na kampuni ya Richmond Development ya Marekani iliyoonekana kutokuwa na uwezo huo.
Akijibu swali kuhusu msimamo wa Chadema wakati wa kashfa hiyo na baada ya Lowassa kuihama CCM, Lissu alisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli amebebeshwa mzigo mzito peke yake.
“Mimi ndiye niliyeandika orodha ya mafisadi na tuliisoma kwa kupokezana na (katibu mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod) Slaa pale Mwembeyanga,” alisema.
“Kile tulichokisema kilithibitishwa na kamati ya (Mbunge wa Kyela, Dk Harrison) Mwakyembe. Je, tuliyosema mwaka 2007 ni uongo? Ukisema uongo, maana yake Richmond haikuwepo. Ukisema kweli maana yake Lowassa alishiriki.
“Kamati ya Mwakyembe ilithibitisha kwamba alishiriki. Sasa amebebeshwa mzigo peke yake. Uamuzi ule ulikuwa wa cabinet (wa Baraza la Mawaziri). Cabinet inaongozwa na Rais. Lowassa aliwajibishwa kwa sababu hakuwasimamia wa chini yake.
“Kuna watu kumi na moja walitajwa na Kamati ya Mwakyembe. Walitakiwa wafukuzwe kazi na washtakiwe. Hadi leo hakuna hatua zilizochukuliwa. Kwa hiyo uwajibikaji wa Lowassa ulikuwa wa kisiasa kwa kuwa alikuwa mtendaji mkuu wa Serikali.”
Lissu alisema hata kamati teule ya Bunge iliyochunguza mkataba huo haikumtaja Lowassa kama mhusika wa moja kwa moja katika kufanikisha kusainiwa mkataba wa Richmond.
“Kitu gani kilitokea kwa (Jakaya) Kikwete aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la mawaziri?” alihoji Lissu
Azungumzia fursa ya upinzani
Akizungumzia nafasi ya upinzani katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020, Lissu alisema vitendo vinavyofanywa na Serikali vinaimarisha upinzani kila uchao.
“Serikali hii ni fursa kubwa kwa upinzania mwaka 2019 na 2020. Fikiria alivyokuwa fursa kubwa Arusha katika uchaguzi wa TLS. Wanasheria walilala kabisa kwa miaka kumi,” alisema Lissu.
“Si wanasheria walioanzisha harakati za vyama vingi? Si kina (Dk Masumbuko) Lamwai, sio kina Mabere Marando walioanzisha NCCR-Mageuzi? Tulipopata vyama vingi wanasheria walienda kulala, utawala wa sasa umewaamsha .”
Katika uchaguzi wa viongozi wa TLS, Lissu alipata ushindi wa asilimia 84 ya kura na kuwabwaga wapinzani wake watatu.
Alisema utawala wa sasa umesaidia kila mmoja kujua umuhimu wa utawala bora, utawala wa sheria, uhuru wa habari na hata umuhimu wa matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge.
Alisema hata wasanii nao wameanza kujitokeza, akisema baadhi wana lugha inayofanana na Chadema ingawa alisema hawafahamu.
Chadema ni chama cha vijana
Kumekuwepo na madai kuwa CCM imekuwa ikiandaa vijana kuwa viongozi wa baadaye, wakati Chadema iking’ang’ania wazee, lakini Lissu anapingana na dhana hiyo.
“Hilo ni tatizo la CCM inayokumbatia vijana waliozima Bunge (waliosababisha Bunge lisirushwe na vituo vya televisheni), waliowasilisha muswada wa habari. Hayo ndiyo malezi?
Alisema inawezekana asilimia 90 ya waliompigia kura Lowassa katika uchaguzi uliopita ni vijana.