Magufuli: Sitaki Mwekezaji Bandarini...!!!!


John Magufuli ameipiga marufuku Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuingia ubia na mwekezaji katika uendeshaji wa bandari hiyo ujenzi wa gati namba mbili utakapomalizika kwa kuwa ujenzi huo umetumia fedha za ndani.

Amesema, ujenzi wa gati jipya katika Bandari ya Mtwara utafungua milango ya kiuchumi na kukuza kipato kwa wakazi wa Mtwara na serikali kwa ujumla.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo jana alipokuwa anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa gati namba 2 katika Bandari ya Mtwara.

Amesema TPA wakiingia mkataba na mwekezaji katika utendaji kazi mara baada ya ujenzi huo kukamilika watakuwa wanainyonya serikali kwa kuwa imejenga miundombinu kwa fedha za ndani.

"Nisisikie hapa tena mmekaribisha mwekezaji...nitashangaa kweli yaani sisi tujenge kwa fedha zetu kisha mlete mwekezaji baada ya kukamilika kwa ujenzi, sitakueleweni kabisa,” ameonya Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema kukamilika kwa ujenzi wa bandari ya Mtwara kutaiwezesha kuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa na nyingi kwa wakati mmoja na hivyo kuharakisha shughuli za upakiaji na ushushaji wa shehena.

Amesema ujenzi wa bandari hiyo utagharimu Sh bilioni 137 na kuchukua miezi 21.

“Naipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kwa kuweza kutekeleza mpango wake wa uboreshaji wa miundombinu ya bandari nchini kwa kuanza na ujenzi wa gati Bandari ya Mtwara" amesema.

“Kukamilika kwa ujenzi wa gati hii kutafungua milango ya kiuchumi na kukuza kipato kwa wakazi wa Mtwara na serikali pia,” amesema Rais Magufuli.

Bandari ya Mtwara ina njia ya kuingilia meli yenye kina cha mita 20 na upana wa mita 250. Meli zenye urefu unaofikia mita 175 zinaweza kutia nanga bandarini bila msaada wa kuvutwa.

Hakuna masharti ya maji kupwa au kujaa kwa meli zinazoingia au kutoka bandarini. Eneo la ndani la kutia nanga lina kina cha mita 20 na uwezo wa kutia nanga meli nne kwa wakati mmoja. Bandari hiyo inayo maeneo ya kuhifadhia mizigo yaliyofunikwa na ya wazi yaliyojengewa ya mita za mraba 11,000 na 15,000 kwa mfuatano huo.

Bandari hiyo pia inashughulikia bidhaa za petroli zilizosafishwa na zisizosafishwa kwa ajili ya kampuni za utafutaji wa mafuta na gesi kupitia kwenye mitambo iliyofungwa upande wa gatini.

Ni kutokana na umuhimu wa bandari hiyo TPA, imeanza kuboresha miundombinu katika bandari hiyo ili kunufaika na fursa kubwa zilizopo katika mkoa huo wa Kusini.

Fursa zilizopo katika mkoa huo na ambazo zinatarajiwa kuinufaisha bandari hiyo ni pamoja na shughuli za watafutaji wa mafuta/gesi, uzalishaji wa gesi asilia na kuhudumia bidhaa zitokanazo na gesi.

Fursa nyingine zilizopo katika mkoa huo ni pamoja na kuhudumia bidhaa za viwanda vinavyojengwa mkoani Mtwara kikiwemo Kiwanda kikubwa cha saruji cha Dangote ambacho kinaendelea na uzalishaji na kuwa tegemeo kubwa kwa uchumi wa Tanzania.

Fursa nyingine ni mazao yanayopatikana Mtwara. Ujenzi wa gati jipya la kisasa katika Bandari ya Mtwara utaiwezesha kuhudumia meli za aina zote zenye urefu wa mita 300.

Ujenzi wa gati hiyopia utasaidia kuongeza ufanisi wa bandari hiyo na kuiwezesha kuhudumia shehena kubwa zaidi ya mizigo. Hadi sasa imethibitika kuwa Bandari ya Mtwara ni moja kati ya bandari zenye usalama zaidi duniani.

Kuhusu utendaji wa bandari hiyo, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2015/2016, shehena iliyohudumiwa katika bandari hiyo ni jumla ya tani 356,356 na 273,882.

Bandari ya Mtwara iliyojengwa miaka ya 1950 ni moja ya bandari zenye maajabu makubwa kutokana na kuwa na sifa ambazo bandari nyingi nchini hazina.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad