Kaimu Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Chunya mkoani Songwe, Benedict Polycap amesema baadhi ya watumishi wanashindwa kufanya kazi kwa utulivu kutokana na kipato chao kupungua baada ya kuanza kukatwa malimbikizo ya mkopo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
Polycap alitoa taarifa hiyo juzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa, kwamba hali hiyo imesbabisha baadhi ya watumishi kupokea mishahara midogo isiyokidhi mahitaji yao hata kwa wiki mbili.
Alisema baadhi ya watumishi wanapokea mishahara kuanzia Sh100,000 hadi Sh200,000, hivyo huamua kujiingiza kwenye shughuli nyingine kutafuta kipato cha ziada ili kujikimu.
Katika tukio jingine, Galawa aliagiza kukamatwa mara moja kwa watumishi wanne wanaodaiwa kugoma kuhamia Halmashauri ya Songwe na kubaki Chunya, huku wakiendelea kupokea mishahara.
Galawa alitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa za idara za halmashauri hiyo. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa watumishi wanne hawajaripoti tangu kuanzishwa kwake Septemba 2016.