UKAIDI! Wakati wakazi mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake wakiendelea kutii bila shuruti agizo la kuacha kunywa pombe, kucheza pool na kamari nyakati za kazi, baadhi ya vijana wakaidi wameonekana kupuuza agizo hilo linalotafsiriwa kama kumchezea sharubu Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda aliyetoa amri hiyo.
Uchunguzi mahususi uliofanywa na Kitengo Maalum cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kimefichua kuendelea kwa michezo ya pool, uchezeshwaji wa kamari na unywaji pombe katika baadhi ya baa na maeneo maarufu, tena vitendo hivyo vikifanyika mchana kweupe.
Katika uchunguzi huo uliofanywa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kama Sinza, Manzese, Temeke, Mbagala na Kariakoo, OFM walishuhudia majira ya kuanzia saa nne asubuhi, katika baa kadhaa, wahudumu wakiendelea na utoaji wa huduma za vilevi bila wasiwasi wowote. Sinza Mori katika baa moja maarufu, ilishuhudiwa baadhi ya watu katika bar hiyo wakiendelea kunywa bia kama kawaida kana kwamba bado wanaishi enzi zile za mwaka 1947.
Kule Manzese, katika baa moja kubwa yenye wateja wengi (majina yao yanahifadhiwa kwa sasa) baadhi ya wateja waliwekwa sehemu ambayo siyo rahisi kuonekana na mtu mgeni, huku wahudumu wakiwapelekea vilevi vyao. OFM ilikuta wanywaji wakipewa bia, pombe kali za kwenye chupa na virobo ambavyo vimepigwa marufuku. Temeke Mwembeyanga, katika baa maarufu eneo hilo, OFM pia walikuta agizo la Mheshimiwa Makonda likipuuzwa mchana wa jua kali, kwani watu waliendelea kupata kile roho inapenda bila hofu yoyote.
Licha ya unywaji wa pombe, pia katika eneo la Mbagala Rangi Tatu, OFM iliwaona baadhi ya vijana wakiendelea na mchezo wa pool bila hofu, licha ya kuwa jua lilikuwa likiwaka, kuashiria muda wa watu kuchapakazi.
Lakini katika hali ya kusikitisha, eneo la katikati ya Kariakoo, kwenye baa moja kubwa ya miaka mingi, pamoja na jua kali la mchana, uuzwaji na unywaji wa pombe ulikuwa ukifanyika pasipo kificho, huku vijana wa rika mbalimbali nao wakionekana wacheza pool, katika meza zaidi ya nne zilizomo ndani ukumbi wa baa hiyo.
Licha ya mitungi, pia baadhi ya wateja waliendelea kucheza kamari ya kwenye vibanda maarufu kama casino pasipo hofu licha ya kwamba baa hiyo ipo umbali wa mita chache tu kutoka kilipo Kituo cha Polisi cha Msimbazi, jijini Dar es Salaam. Licha ya Makonda kutoa amri ya kuachwa kwa vitendo hivyo wakati wa saa za kazi, pia viongozi wengine wa ngazi za ukuu wa wilaya, mikoa na mawaziri, wamewahi kutoa maagizo ya kutochezwa kwa pool, kunywa pombe na hata kwa wamiliki wa maeneo yanayoendesha shughuli hizo kufungwa nyakati za kazi.