Zipo sauti nyingi zinapazwa kuwa kelele za cheti zinasababishwa na vita ya wauza dawa za kulevya. Sikubaliani na hoja hiyo, ingawa naweza kukubali kwamba watu wasiompenda Makonda kwa sasa wamepata fimbo ya kumcharaza hasimu wao.
Usiseme vita ya wauza dawa za kulevya ni ngumu ili kuhalalisha cheti bandia cha Makonda kama kweli anacho. Mtetee Makonda kwa kujibu hoja zote zinazotolewa. Kwamba safari nzima ya kielimu ya Makonda ni halali na haina doa. Huo ndiyo utetezi unaopaswa kutolewa kwa wakati huu.
Hao wauza dawa za kulevya ni akina nani mpaka wawe huru kumshambulia Makonda? Huu ni utoto ambao kwa watu wenye fikra timamu wanajisikia vibaya kuusikia ukisemwa kumtetea Makonda.
Kama kweli Makonda alighushi cheti, basi dhambi yake isifunikwe kwa kisingizio cha wauza dawa za kulevya. Uhalifu mmoja siyo pepo ya uhalifu mwingine.
Uhalifu wa kughushi cheti siyo pepo dhidi ya uhalifu wa biashara haramu ya dawa za kulevya. Wote ni uhalifu. Kwa hiyo dhambi ya kughushi cheti ya Makonda (kama kweli ameitenda), haipaswi kufichwa kwenye kivuli cha mapambano ya dawa za kulevya.
Kwanza muuza unga gani huyo anayepambana na Makonda? Maana wote aliowataja wapo mitaani, hakuna hata mmoja ambaye alithibitika.
Hivyo basi, kusema Makonda anashambuliwa na wauza unga ni kuwaonea wale waliotajwa kisha wakabainika kuwa hawahusiki. Watu wasihukumiwe kwa makosa ambayo hayajathibitishwa na mahakama.
Tena kwa maneno haya ni matusi hata kwa Serikali, kwamba wauza unga walikamatwa, wakaishinda Serikali na sasa wanaendesha vita dhidi ya Makonda. Haya siyo maneno mazuri kuzungumzwa.
Nayasema haya kuweka sawa huu mjadala. Ni vizuri hasa Makonda ajitetee na ashinde hii vita dhidi yake ili kama kijana awe na safari njema ya kiuongozi. Na kama ni kweli dhambi inayotajwa kaitenda, basi vita ya dawa za kulevya isiwe chimbo la kujifichia.
Ndimi Luqman MALOTO
ATOE VYETI KAMA WALIVYOFANYA WENGINE ILI KELELE ZIISHE! WATU WA MWANZA NA KIJIJINI KWA BASHITE, WANAJUA YEYE ANAITWA DAUDI... AWEKE VYETI AACHE KELELE
ReplyDelete