Mfanyabiashara Akurupushwa Porini Akichinja Mizoga ya Punda


Kweli ni hatari kubwa! Wabongo wanakula vingi ambavyo hawavijui vilikotoka hali inayohatarisha afya zao! Hilo limedhihirika Machi 6, mwaka huu kuuatia mfanyabiashara mmoja ambaye hakujulikana jina mara moja, mkoani hapa kukurupushwa porini baada ya kukutwa akiwa anachuna mizoga ya mnyama punda ambaye haikujuli  kaka aliwaua kwa mtindo gani.     

Tukio hilo la kushangaza, lilijiri kwenye pori la Kijiji cha Kidomole  wilayani Bagamoyo mkoani hapa ambapo, Amani lilibahatika kukuta mizoga hiyo baada ya mtuhumiwa kukimbia.

Kwa mujibu wa wafugaji wa eneo hilo ambao ni Wamasai, siku ya tukio, walipata taarifa kutoka kwa mwanamke aliyejulikana kwa jina moja la Maria kwamba punda wake wawili wamepotea ndipo walipoanza msako wa kuwasaka wanyama hao.

“Sasa tukiwa tunaendelea kuwasaka, mara tukafika kwenye pori hilo na kumkuta bwana mmoja anawachuna wale punda. Khaa! Tukashangaa sana. Lakini kabla hatujamkamata alikimbia. “Kusema ukweli licha ya kwamba alikimbia lakini kwa sura tunamjua vizuri sana. Ni mfanyabiashara wa nyama Bagamoyo. Ni muuza nyama ya ng’ombe.

Sasa kuna uwezekano kumbe zinakuwaga si nyama za ngo’mbe bali ni punda kwani huku wanyama  hao wanapotea mara kwa mara,” alisema mfugaji mmoja bila kutaja jina lake. Mfugaji huyo aliongeza kuwa, mtuhumiwa amekuwa akipeleka nyama maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuziuza. Sehemu hizo ni pamoja na Chalinze, Bagamoyo yenyewe na jijini Dar es Salaam.

Mfugaji huyo aliendelea kudai kuwa, kwa sababu wanamfahamu mtuhumiwa huyo hivyo wanajipanga kwenda kutoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Bagamoyo ili akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Akizungumza na Amani, Maria ambaye ndiye mmiliki wa punda hao alisema:

“Kwa kweli nimeumia sana kwani punda walikuwa wakinisaidia kubeba mizigo, kwenda kuchota maji, sasa wamewaua mimi nitafanya nini?” Baadhi ya watu walioshuhudia  tukio hilo walisema kuwa, baadhi ya watu wanakula nyama ya punda, wengine hawali.

Wakasema kuwa wana hofu mtuhumiwa huyo huichukua nyama hiyo na kutangaza kwamba ni ya ng’ombe na kuwalisha watu mishikaki yake.

“Mbaya zaidi, nyama yenyewe hakuna cha kupimwa wala kuangaliwa kama mnyama alikuwa mzima kiafya au la! Hii ni hatari sana.

Huyu mtu akamatwe mara moja na kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Huwezi kuwalisha binadamu wenzako nyama ambayo wao hawaitumii. Kama kwake ni halali, kwa wengine ni haramu,” alisema Mathayo, mkazi wa Bagamoyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad