WAKATI ikiwa ni mwaka wa pili tangu kufariki dunia kwa aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba,
Imefahamika kuwa mjane wa kada na mtumishi huyo wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salome Komba, yungali katika wakati mgumu hivi sasa baada ya kuzungushwa na chama hicho kila uchao kuhusiana na mafao ya marehemu mumewe.
Aidha, kwa kipindi chote tangu kufariki kwa Komba, Salome amelipwa Sh. milioni 4.5 tu ikiwa ni sehemu ya mafao hayo anayodai kuwa jumla yake ni Sh. milioni 75.
Kabla ya kuwa mbunge mwaka 2005, na hata baada ya hapo, Komba alikuwa akiitumikia CCM kwa nafasi mbalimbali ikiwamo ya kuwa mkurugenzi wa kikundi cha sanaa cha TOT (Tanzania One Theatre) kinachomilikiwa na CCM na kuwa mhimili wa uhamasishaji hasa nyakati za kampeni za uchaguzi.
Wimbo “Wataisoma Namba” uliotikisa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ni zao mojawapo la tungo zilizotikisa za marehemu Komba na hivi sasa, baadhi ya watu hutumia maudhui ya wimbo huo kuelezea kimzaha hali anayokutana nayo mtu pindi anapokumbana na changamoto za kifedha; ingawa lengo halisi la wimbo huo huonekana kuwa ni kuwapiga vijembe wapinzani wa CCM wenye kawaida ya kubeza kila kizuri kinachofanywa na chama tawala.