Mmiliki wa Kona Baa Atoa ya Moyoni Baada ya Kufungiwa


DAR ES SALAAM: Mmiliki wa baa maarufu iliyopo katika viunga vya mitaa ya Sinza maarufu kama Kona Baa, Joseph Mushi ametoa ya moyoni kuhusu sakata la kufungiwa kwa baa yake na Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko kwa masikitiko juzi, Mushi alisema anashangazwa na hatua ya serikali kuifunga baa yake kwa kigezo kwamba kuna biashara ya ukahaba kwenye baa hiyo. “Biashara yangu hapa ni kuuza vinywaji mbalimbali, nahudumia wateja tofauti kwa kuzingatia rika na sheria zilizowekwa, siwezi kumjua mtu fulani anajiuza na huyu hajiuzi, jambo hilo linabaki kuwa suala la mtu binafsi.

“Ni kweli nimekuwa nikisikia na wakati mwingine kuona kuna dalili za kuwepo kwa vitendo vya biashara ya namna hiyo, hata hivyo nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha natokomeza uwepo wa shughuli hizo.

“Nimekuwa ni mtu wa kwanza kununua magari mawili pamoja na pikipiki moja na kuzikabidhi kwa jeshi la polisi kanda maalumu enzi hizo kitengo hicho kikiwa chini ya Kamanda Kova (Suleiman) ili kuweza kutusaidia kuwakamata madada poa wote wanaozunguka eneo hili sanjari na wahalifu wengine wa makosa mbalimbali.

“Niiombe serikali kutazama njia nyingine za kukabiliana na tatizo la ukahaba nchini pasipo kuathiri shughuli zetu za kiuchumi, ifahamike kupitia kazi hii nimeajiri Watanzania wengi ambao wamekuwa wakijipatia kipato cha kuyaendesha maisha yao, hivyo kwa kufungia biashara hii siyo tu itaniathiri mimi peke yangu lakini pia Watazania wengi,” alisema Mushi.

Aidha, katika hatua nyingine, madereva bodaboda wa eneo hilo wamesema tangu kufungiwa kwa baa hiyo, hali ya biashara imekuwa mbaya kwani wateja wao wengi walikuwa ni wale waliokuwa wanaburudika katika baa hiyo. “Hali ni mbaya kwa sasa, nilikuwa nafanya kazi eneo hili napata shilingi elfu kumi na tano hadi ishirini kwa siku, sasa hivi hata kuipata shilingi elfu kumi ni tabu,” alisema dereva bodaboda mmoja ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini.

Pamoja na hayo, majirani wa mitaa hiyo, waliunga mkono serikali kwa kitendo cha kuifungia baa hiyo kwa madai kwamba hiyo imekuwa chanzo cha kuharibu watoto wao kimaadili. “Hii baa imekuwa kero mtaa huu kwa muda mrefu, wao hawajali huyu ni mtoto, wanachojali wao ni pesa, watoto wadogo wanajiuza, wanacheza muziki na kunywa pombe bila kuogopa chochote, kwa kweli mimi naona ni sahihi kwa uamuzi wa serikali,” alisema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad