Mtaji wa Godbless Lema ni Dola...


Hapa Lema wala sitaki kukupamba kinafiki. Siamini hata kidogo kuwa wewe ndiye hasa unatakiwa kuwa mbunge maarufu zaidi, nikipima michango yako ndani na nje ya Bunge.

Kama ingekuwa unapimwa kwa hoja zako za ndani ya Bunge au hata nje, ungebaki kuwa mbunge wa kawaida, japo sisemi wewe huna athari bungeni. Athari unayo, tena kubwa, ila wapo ambao wanakuzidi bungeni lakini unawameza nje ya Bunge.

Lema, wewe mtaji wako ni dola. Kadiri dola inavyotumia nguvu kukudhibiti ndivyo na wewe unavyopaa kwa umaarufu. Utaendelea kuitesa na utazidi kuitumia kama ngazi ya kupaa kwako kisiasa kama haitajishitukia na kujirekebisha.

Nguvu haijawahi kuwa nyenzo bora ya mapambano kama akili haipewi ushiriki wa kutosha. Mabavu bila kushirikisha ubongo matokeo yake ni kuua mende kwa shoka kwenye marumaru. Mwisho muuaji kugeuka kichekesho.

Yapo mambo ambayo kweli hayakuwa na maana yoyote wewe kuyatamka, lakini jinsi ambavyo nguvu kubwa imetumika kukushughulikia, ndiyo inayowafanya watu kusahau makosa yako na kuishia kukuhurumia, huku wakiwafikiria watumia nguvu kwa pupa bila kupata majibu.

Kama wangekuwa wanatumia kiasi cha nguvu sawasawa na kosa husika, pengine hali isingekuwa kama ilivyo sasa. Tatizo wanaamini mno mamlaka. Hawajui kuwa mamlaka yameelekezwa kufuata sheria. Tanzania ni nchi ya utawala wa sheria.

Kufikia sasa, jina lako halizungumzwi Tanzania tu, bali ulimwengu umeambiwa mengi kuhusu msoto wako wa dhamana. Utaona kuwa jina lako linakua zaidi. Maana yake nguvu za dola zimekuwa daraja la kupaisha jina lako mpaka anga nyingine.

Ndimi Luqman MALOTO

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kwa hiyo unamaanisha atukane wakuu wa nchi asishughulikiwe ama kweli sie wabongo tuna akili mgando ingekuwa hizi akili tunazitumia kwa masilahi ya maana nchi ingefika mbali sana lakini tatizo tumejaliwa ni mafundi kutumia akili na nguvu nyingi kupindisha yaliyo kweli sasa eti Lema anapandishwa kisiasa ni mtaji kwa kushughulikiwa na makosa ayafanyao tunamsifia anakomazwa tobbaaaaa

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hakika unachosema, inashangaza watu kumpongeza mtu anayetukana watu wengine na kulaumu mamlaka pale mtu huyo anapochukuliwa hatua. Uko sahihi unaposema wana akili Mgando, well said.

      Delete

Top Post Ad

Below Post Ad