Mtafiti wa viumbe hai na mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Bayreuth cha nchini Ujerumani, Dk Andrew Hemp ameelezea sifa za mti ujulikanao kama Mkukusu kuwa unaweza kuishi kati ya miaka 200 hadi 300, lakini ulioonekana nchini una miaka 600.
Akiuzungumzia mti huo ambao unapatikana katika Kijiji cha Tema wilayani Moshi, mtafiti huyo amesema mti huo ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika una urefu wa mita 81.5 na uko katika eneo lililopo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa).
Dk Andrew amesema kwa mujibu wa utafiti mti huo una uwezo wa kuishi miaka hiyo kwa kutunzwa na kuhifadhiwa.
Amesema kwamba katika utafiti walioufanya barani Afrika waligundua miti mirefu 31, lakini Mkukusu wa Moshi ndiyo mrefu kuliko yote na una umri wa miaka 600 hivi sasa ukiwa umevuka kiwango cha juu cha maisha ya miti ya aina hiyo.
Tayari Serikali imeiagiza Kinapa kuboresha miundombinu ya barabara ili kuweza kuufikia mti huo iwapo watalii watataka kwenda kuuona.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki amesema mti huo utasaidia kuongeza mapato kwa kasi kwa kuwa ni kivutio kipya cha utalii ndani ya mkoa huu.