Makonda hakuwa sahihi kumtaja Gwajima kuwa anahusika na dawa za kulevya wakati hakuwa na ushahidi angalau wa asilimia 90. Kitendo cha Gwajima kutofunguliwa mashitaka, maana yake alimtaja bila ushahidi.
Gwajima hapaswi kuendesha vita yake binafsi na Makonda kupitia Kanisa. Ni kama ambavyo Makonda hakuwa sawa kutumia cheo chake kumpa Gwajima tuhuma nzito za dawa za kulevya.
Tafsiri ni kuwa Makonda alitumia ofisi yake vibaya, naye Gwajima ametumia madhabahu yake vibaya. Kwa msemo wa mtaani, hiyo wanaita “mbwa kala mbwa! Yaani mechi sare. Kwamba ngoma droo.
Wanasheria wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao katika kesi, hufanya marejeo ya kesi za nyuma zenye mfanano na kesi husika ili kuzipa uzito hoja au hukumu, wenyewe huita legal citation.
Kwa kesi hii, ‘legal citation’ ambayo naitumia ni tukio la miaka nane iliyopita, pale mfanyabiashara Reginald Mengi alipotangaza wafanyabiashara watano kuwa ndiyo mafisadi papa. Aliwataja kuwa ni Rostam Aziz, Yusuf Manji, Tanil Somaiya, Jeetu Patel na Subhash Patel.
Rostam alimjibu Mengi kwa kumtaja kuwa ni fisadi nyangumi. Baada ya hapo mzee Mengi alikwenda mahakamani, akituhumu kuchafuliwa jina lake.
Swali likawa, je, kwani wakati yeye anataja mafisadi papa, alidhani Rostam angechekelea na asingeumia? Kila nafsi ina nyama na damu, kinachokuumiza wewe, na mwenzako akitendewa kitamuumiza.
Kama ambavyo Makonda anaumia na hata kutoa machozi kwa sababu ya mjadala wa cheti, ndivyo na Gwajima aliumia sana kutajwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya. Zaidi Gwajima alilala mahabusu, akapelekwa nyumbani kupekuliwa kisha kupimwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Gwajima hakulia ila aliumia.
Kinachotokea kati ya Makonda na Gwajima, ni ile dhana kuwa ukichezewa rafu uwanjani kisha ukarudisha, wewe unakuwa umekosea zaidi. Hata hivyo ukweli usiopingika ni kuwa anayetumia mamlaka ya nchi kumkabili raia isivyofaa, anapaswa kuwa mkosefu zaidi.
Kwa msingi huo, watu wanaomlaumu Gwajima kutumia uwanja wa taasisi yake ya kidini kumkabili Makonda, wanatakiwa kuwa wakali zaidi kumsema Makonda kutumia ofisi ya umma kuzushia watu kashfa na kuwachonganisha na jamii
By @luqmanmaloto
Gwajima hajasingiziwa,Inapendeza mtumishi wa Mungu kutubu,aseme alishafanya ila kwa sasa kaacha.Utajiri wake unatokana na sembe.
ReplyDelete