Nape Nhauye: Nitamlinda mwekezaji wa Radio E-FM

WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, ameahidi kulinda uwekezaji wa mmiliki wa kituo cha Redio EFM na Tv E, Francis Ciza, maarufu Dj Majizo.

Nape alitoa kauli hiyo jana wakati alipotembelea makao makuu ya kituo hicho cha redio katika eneo la Kawe, Dar es Salaam.

Katika hotuba yake fupi aliyoitoa mbele ya watumishi wa redio hiyo jana, Nape alisema yeye ndiye waziri mwenye dhamana ya habari, hivyo ana wajibu wa kulinda habari na wawekezaji katika tasnia hiyo.

“Nataka nikuhakikishie mimi ndie waziri mwenye dhamana ya habari, kuilinda habari na tasnia yenyewe, lakini kuwalinda wanaowekeza kwenye tasnia hii, kwa sababu uwekezaji kama huu ulioufanya katika tasnia hii, ndio unanifanya mimi kama waziri niendelee kuwapo.

“Lakini ndio unaoifanya Serikali na Tanzania kuendelea kuwa nchi njema ya watu waendelee kuishi, kazi yako ni nzuri na nyinyi kwa kuwa mnasikika sana Dar es Salaam, mchango wenu wa kuifanya Dar es Salaam kuwa njema ni mkubwa na hauwezi kupuuzwa hata kidogo.

“Kwa mtu yeyote mwenye mapenzi mema na Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla atawalindeni, atawalinda na kuhakikisha mnapata ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yenu,” alisema.

Nape pia alimpongeza Majizo kwa uwekezaji mkubwa alioufanya na kuahidi kwamba serikali itampatia ushirikiano na msaada anaouhitaji ili kuhakikisha uwekezaji wake unasonga mbele.

“Kama Serikali na kama waziri mwenye dhamana ya habari, nimeshuhudia kwa macho yangu uwekezaji uliouweka hapa, tutalinda uwekezaji uliouweka usiharibiwe ovyo.

“Si Watanzania wengi wenye maono haya, najua umeanza mbali mpaka kufika hapa, si kazi rahisi, ndiyo maana nasema ukiona mtu kasimama si vizuri kwenda kumparamia ovyo.

“Ni vizuri kuheshimu kazi ambayo amehangaika nayo, jasho si la bure, uwekezaji huu ni mkubwa sana, labda iwe hujui alichowekeza, hujui kapambana kiasi gani kufika hapo ndiyo unaweza kufanya unachotaka,” alisema Nape.

 Nape alisema katika dunia yenye ushindani vita ni kubwa, hivyo akamtaka mwekezaji huyo asikatishwe tamaa na kelele za barabarani kwa sababu Serikali iko pamoja naye.

Aliwaeleza pia watumishi wa redio hiyo kwamba wasiwe na hofu kwa sababu kazi wanayoifanya ina baraka za Mungu, hivyo hawapaswi kuvunjika moyo.

“Mkiona mti unaotupiwa mawe ni ule wenye matunda, kwa miaka mitatu mafanikio mliyoyapata ni makubwa sana, lazima yatamtisha yule aliepo sokoni, kwahiyo mkiona kuna vita basi mjue ni kwa sababu kasi yenu ni kubwa mno kiasi kwamba inawatia joto wengine.

“Mtu mmoja aliwahi kuniambia wakati naanza siasa kwamba ukiona watu hawakuzungumzii jiulize kama bado unaishi au umeishakufa, ukiona watu wanakuzungumza ujue umewazidi,” alisema Nape.

Majizo ni mmoja wa watu waliohusishwa na dawa za kulevya katika kampeni iliyokuwa ikiendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad