Ndoto za mshambuliaji wa timu ya KRC Genk ya Ubelgiji Mtanzania Mbwana Samatta za kukanyaga katika dimba la Old Trafford la Manchester United zimesubirishwa baada ya matokeo ya droo ya robo fainali kombe la Europa kwenda kinyume na matamanio yake.
Hamu ya Nahodha huyo wa Taifa Stars ilikuwa ni kuona timu yake ya Genk inapangwa kukutana na Man United katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, ili atimize ndoto yake mojawapo ya kucheza katika uwanja wa huo maarufu na uliotoa mastaa wengi duniani.
Samatta baada ya mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ambao timu yake iliibuka na ushindi wa 5-2 na kutoa nafasi kubwa ya kufuzu robo fainali, alinukuliwa akisema "Moja kati ya ndoto zangu ni kukanyaga katika dimba la Old Trafford, kwahiyo naomba kila siku timu yetu ikivuka, ipangwe na Manchester United"
Hata hivyo, katika droo iliyochezeshwa leo, KRC Genk imepangwa kuanzia nchini Hispania dhidi ya Celta Vigo, na mchezo wa marudiano utapigwa nchini Ubelgiji.
Ili timu hiyo ikutane na Man United msimu huu, inapaswa kwanza kuitoa Celta Vigo, huku ikiomba Man UNited pia ifuzu nusu fainali, halafu droo iwakutanishe.
Kutokana na ukweli kwamba timu ya Man United ndiyo yenye mashabiki wengi zaidi duniani, ingeweza kuwa ni fursa adhimu kwa Samatta kujitangaza zaidi, kwa kuwa watu wengi hawapitwi kutazama mchezo wowote unaoihusu timu hiyo iliyo chii ya kocha Jose Mourinho