Ngoma Huyoo Msimbazi,Wakala Wake Afunguka Mchezo Mzima Jinsi Ulivyo..!!!


HII unaweza ukaihesabu kama ni vita mpya baina ya mahasimu wa soka nchini, Simba na Yanga.

Hali hiyo inaletwa na mkakati wa siri ambao Dimba imeugundua ambapo vigogo wa timu ya Simba wameamua kuingia vitani kumshawishi na kisha kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Donald Ngoma, muda mfupi baada ya kumaliza mkataba wa kuitumikia timu hiyo ya Jangwani.

Ngoma, ambaye ni raia wa Zimbabwe, anamaliza mkataba wake sambamba na kuhitimishwa kwa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara Mei, mwaka huu.

Habari za uhakika ambazo Dimba limezipata kutoka kwa mmoja wa viongozi waliokuwamo katika kamati ya usajili zilisema kwamba, mchezaji huyo anapigiwa mahesabu na klabu hiyo ya Msimbazi kutokana na uwezo wake anaoendelea kuuonyasha katika klabu ya Yanga.

Mjumbe huyo alibainisha kuwa, hata hivyo, klabu yake inamtaka straika huyo siyo kwa ajili ya kucheza michuano ya Ligi Kuu, bali wanamtaka kwa ajili ya kuiongezea nguvu timu hiyo katika michuano ya kimataifa, ambapo wenyewe Simba wanaamini watatwaa ubingwa msimu huu na hivyo watakuwa wakishiriki michuano hiyo hapo mwakani.

Mjumbe huyo amekwenda mbali zaidi na kudai kwamba, tayari dau la mshambuliaji huyo limeshawekwa mezani ambapo Wekundu hao wa Msimbazi watatakiwa kulipa kiasi cha Dola za Kimarekani 150,000, sawa na Sh milioni 300 za Kitanzania ili kuweza kumnasa Mzimbabwe huyo.

“Kiasi hicho tunaweza kutoa, lakini hii itawezekana endapo tutapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa hapo mwakani,” alisema.

Wakala wa mchezaji huyo, Jonas Tiboroha, alikiri kupigiwa simu na kigogo mmoja wa Simba, ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake na kuomba taratibu za kumsajili mchezaji huyo.

Tiboroha alisema, licha ya Simba, pia klabu za Mamelodi Sandown, Malaga FC za Afrika Kusini, Zesco ya Zambia, Al Ahly ya Misri zimeonyesha nia ya kumhitaji mshambuliaji huyo, lakini pia klabu yake ya sasa, Yanga nao wameshaonyesha nia yao ya kumbakiza mshambuliaji wao huyo ambaye hadi sasa ameshaipachikia timu yake hiyo mabao 8 katika michuano ya Ligi Kuu.

Alisema, Yanga wameweka ofa ya Sh milioni 120, kwa ajili ya mkataba mpya wa Mzibambwe huyo baada ya ule wa kwanza kumalizika.

Katika hatua nyingine, vigogo karibu wote wa klabu ya Simba wiki iliyopita walikutana kwa siri katika sehemu nyeti inayofahamika kwa jina la Pentagoni, iliyopo maeneo ya daraja la Salenda, katikati ya jiji la Dar, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili na kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanachukua pointi zote 18 zilizobaki ili waweze kuchukua ubingwa msimu huu.

Vigogo hao wa kamati ya utendaji pamoja na wadau wengine, wakiongozwa na Rais wa klabu hiyo, Evance Aveva, wamekuwa wakikutana mara kwa mara katika kipindi hiki ambacho timu yao iko kileleni katika msimamo wa ligi, huku wakielekea kusafiri kwenda kanda ya ziwa kwa ajili ya kucheza mechi tatu ambazo ndizo zitakazotoa mwanga wa timu hiyo kutwaa ubingwa au la.

Hata hivyo, Aveva aliliambia Dimba kwamba, kukutana kwao ni kawaida kama viongozi na wadau kwa ajili ya kujadili maendeleo ya timu yao, lakini bado kikosi chao hicho kitakuwa na mikakati ya kifundi inayoendelea kuandaliwa na benchi la ufundi chini ya kocha wake mkuu, Joseph Omog.

“Kocha ndiye anayejua masuala ya ufundi, ukisikia sisi tukikutana ujue tunapanga mikakati mingine, maana klabu si wachezaji pekee, bali na viongozi pia wana majukumu ya kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.

Naye Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amesema katika wakati wowote aliokuwa akiifundisha Simba, kipindi hiki ndicho kinachomuweka katika wakati mgumu, hasa kutokana na umuhimu wake.

Kocha huyo aliliambia Dimba kwamba, anafahamu mechi zilizobaki ni ngumu, hivyo miongoni mwa mambo muhimu anayotakiwa kuyahakikisha ni kuwaweka vijana wake katika hali ya tahadhari ili wasijiachie wakadharau mechi zilizosalia.

Endapo ratiba haitabadilika Simba itakipiga na Kagera Sugar Aprili 4, mwezi ujao na kisha itakwenda jijini Mwanza kukipiga na Toto Africans na kisha itacheza na Mbao, mechi ambazo kocha huyo alisema ni ngumu na zinazohitaji mikakati ya nguvu.

Mpaka sasa Simba ndiyo inayoongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 55, ikifuatiwa kwa karibu na watani wao wa jadi, Yanga, iliyofikisha Pointi 53, huku zote zikiwa zimeshacheza michezo 24.

Credit - Dimba

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad